Dec 12, 2025 02:37 UTC
  • Ijumaa, Disemba 12, 2025

Leo ni Ijumaa tarehe 21 Mfunguo Tisa Jumadithani 1447 Hijria inayosadifiana na tarehe 12 Disemba 2025.

Siku kama ya leo miaka 1063 iliyopita yaani sawa na tarehe 21 Jamadithani mwaka 384 Hijiria, kwa mujibu wa baadhi ya kauli za kihistoria, alifariki dunia Muhsin Bin Ali Tanukhi, mtaalamu wa fasihi, malenga na mwanahistoria mashuhuri wa Kiislamu.

Tanukhi alikuwa na kipawa katika uga wa kuhifadhi mashairi na fasihi ambapo ameacha turathi kubwa ya mashairi. Kwa muda mfupi, Muhsin Bin Ali Tanukhi alikwea hatua za kielimu na kidini katika zama zake na kujishughulisha na kazi ya ukadhi.

Kitabu cha ‘al Faraj Baada Shiddat’ kinachozungumzia matukio ya kihistoria na kijamii ya zama zake, ni miongoni mwa athari zilizoandikwa na msomi huyo. Kitabu kingine cha msomi huyo ni ‘Al-Masaajid’ ambacho kinakusanya hekaya na masuala ya akhlaqi na maadili mema.

Katika siku kama ya leo miaka 204 iliyopita, alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Kifaransa, Gustave Flaubert katika mji wa Rouen nchini Ufaransa.

Alipenda sana taaluma na fasihi akiwa bado kijana na kwa sababu hiyo aliacha masomo ya sheria, akaondoka Paris na kwenda kuishi maeneo ya vijijini. Wakati huo ndipo alipoandika vitabu vilivyompa umashuhuri mkubwa.

Japokuwa Gustave Flaubert hakuandika vitabu vingi lakini athari na vitabu vichache vya mwandishi huyo vinahesabiwa kuwa vya aina yake katika taaluma ya fasihi duniani.

Vitabu mashuhuri zaidi ya Gustave Flaubert ni Madame Bovary, Sentimental Education na Three Tales. Flaubert aliaga dunia tarehe 8 Mei mwaka 1880 akiwa na umri wa miaka 59. 

Tarehe 12 Disemba miaka 136 iliyopita, alifariki dunia Robert Browning, malenga na mwanafikra wa wa Uingereza akiwa na umri wa miaka 77.

Akiwa kijana mdogo Browning alikuwa na maandalizi ya kuwa malenga ambapo alitoa shairi lake la kwanza akiwa na umri wa miaka 12. Taratibu akaanza kupata umashuhuri katika jamii ya Uingereza kama malenga mkubwa. Robert Browning alikuwa akiwasilisha itikadi yake kuhusuu dini na Mwenyezi Mungu kupitia mashairi yake.

Ameacha athari nyingi katika uwanja huo. Robert Browning alifariki dunia mwaka 1889.   

Miaka 124 iliyopita katika siku kama ya leo, kulianza ukurasa mpya katika historia ya mawasiliano ya mwanadamu baada ya kuzinduliwa mawasiliano ya njia ya mawimbi ya redio bila ya kutumiwa nyaya.

Tukio hilo lilifanyika kwa kuwasiliana kwa maneno kutoka eneo moja la Italia kwenda jingine. Mtu aliyetumia mawasiliano ya aina hiyo kwa mara ya kwanza alikuwa mwanafizikia wa Italia Guglielmo Marconi  ambaye baadaye alivumbua pia redio.

Hii leo vyombo vya mawasiliano vinavyotumia mawimbi ya redio vinatumiwa katika masuala mengi duniani. 

Tarehe 12 Disemba 1963, yaani siku kama hii ya leo miaka 62 iliyopita, Kenya ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza.

Kenya ilianza kuvamiwa na Waingereza mwanzoni mwa karne ya 20 na mwaka 1920 ikakoloniwa rasmi. Harakati ya wananchi iliyoongozwa na Jomo Kenyata ilipambana na wakoloni hao katika vuguvugu la kupigania uhuru dhidi ya Uingereza. Hatua ya wazungu hao wakoloni ya kuhodhi madaraka ya nchi na mivutano ya ndani vilikaribia kuitumbukiza Kenya katika mapigano ya ndani katika muongo wa 1950.

Baada ya kupamba moto wimbi la kupigania uhuru la wazalendo wa Kenya, kulipasishwa katiba ambayo ilidhamini usawa wa watu wa rangi zote nchini humo.

Nchi hiyo ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza tarehe 12 Disemba 1963 chini ya uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta na siku hii inajulikana kwa jina la Jamhuri Day au Siku ya Jamhuri.