Jumanne, tarehe 18 Agosti, 2026
Leo ni Jumanne tarehe 5 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1448 Hiijria sawa na tarehe 18 Agosti 2026.
Siku kama ya leo miaka 1373 iliyopita, vilitokea vita vya Ajnadeen katika eneo la Ajnadeen huko Palestina kati ya Waislamu na Warumi.
Katika vita hivyo ambavyo havikuwa na mlingano hasa kwa kuzingatia kuwa, askari wa Kirumi walikuwa wengi mara kadhaa kuliko Waislamu, jeshi la Waislamu liliibuka na ushindi mkubwa kutokana na wapiganaji wake kuwa na irada na imani thabiti.
Baada ya Warumi kushindwa vibaya na Waislamu waliamua kurejea nyuma hadi katika mpaka wa Palestina na Syria sambamba na kupoteza maeneo mengi yaliyokuwa chini ya udhibiti wao. ***
Miaka 180 iliyopita katika siku kama ya leo, tarehe 5 Rabiul Awwal 1268 Hijria, kilifunguliwa Chuo Kikuu cha kwanza cha Kiirani kwa mtindo wa kisasa.
Chuo hicho kilichojulikana kwa jina la 'Darul Funun' kilianza kutoa mafunzo katika zama za Ufalme wa Naasiruddin Shah Qajar. Lengo la kuanzishwa chuo hicho lilikuwa kustawisha sayansi na elimu ya kisasa hapa nchini. ***
Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, alifariki dunia Muhammad Ghaffari aliyekuwa na lakabu ya Kamal al-Mulk mchoraji mahiri wa Kiirani. Alisoma katika skuli ya Darul Funun ya Tehran na kupata mafanikio makubwa katika fani ya uchoraji aliyokuwa akiipenda. Kipindi fulani Muhammad Ghaffar alifanya kazi katika utawala wa Nasser Deen Shah Qajar na kufanikiwa kutoa athari zenye thamani kubwa za uchoraji. ****
Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 18 Agosti 1964, Afrika Kusini ilipigwa marufuku kushiriki kwenye mashindano ya 18 ya Olimpiki yaliyofanyika Tokyo huko Japan, baada ya kukataa kulaani vitendo vyake vya ubaguzi wa rangi dhidi ya wazalendo weusi nchini humo. Uamuzi huo ulichukuliwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) baada ya kumaliza kikao chake huko Lausanne, Uswisi. Ujumbe wa Afrika Kusini ulisusia kikao hicho. ***
Mnamo tarehe 18 Agosti mwaka 1977, mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini, Steve Biko, alikamatwa na utawala wa ubaguzi wa rangi.
Biko alikamatwa baada ya kusimamishwa kwenye kizuizi cha barabarani akiwa na Peter Jones, walipokuwa wakisafiri kwenda Cape Town. Steve Biko alifariki dunia akiwa chini ya ulinzi wa polisi mnamo Septemba 12, 1977, kutokana na majeraha aliyopata wakati wa kuhojiwa.
Biko, aliyekuwa mwanaharakati mashuhuri wa kupinga ubaguzi wa rangi na kiongozi wa Black Consciousness Movement, aliwahi kuzuiliwa na kuwekewa vikwazo na serikali ya ubaguzi wa rangi mara kadhaa.
Kukamatwa huko na baadaye kifo chake, viliibua hasira na kulaaniwa kimataifa. ***
Katika siku kama hii ya leo miaka 47 iliyopita Imam Ruhullah Khomeini alitoa amri ya kuvunjwa mzingiro na kukombolewa eneo la mpakani la Paveh huko Magharibi mwa Iran.
Eneo hilo lilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na baadhi ya makundi yaliyokuwa yakipiga vita Mapinduzi ya Kiislamu. Makundi hayo yalikuwa yakisaidiwa na madola ya kigeni na yalianzisha machafuko katika maeneo mbalimbali ya Iran baada tu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.
Baada ya amri hiyo ya Imam Khomeini wananchi na wanajeshi waliharakia kwenda eneo la Paveh na kulikomboa kikamilivu. ***
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, baada ya vita vya miaka minane vya kulazimishwa Iran na Iraq, hatimaye Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi kusimamishwa vita hivyo kwa mujibu wa moja ya vipengee vya azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la umoja huo.
Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, madola yanayopenda kujitanua ambayo yaliona maslahi yao yamo hatarini hapa nchini yalianza kutekeleza njama mbalimbali ili kuuangusha mfumo wa Kiislamu wa Iran.
Saddam Hussein, kibaraka wa madola ya Magharibi na hasa Marekani, wakati huo akiwa Rais wa Iraq alitumiwa na Washington na kuanzisha vita vya miaka minane dhidi ya taifa la Iran akitumia visingizo visivyo na msingi wowote.
Mwanzoni mwa vita hivyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio la kutaka kusimamishwa vita hivyo, ingawa cha kusikitisha katika azimio hilo ni kwamba, baraza hilo halikuashiria hata kidogo uchokozi wa majeshi vamizi ya Iraq dhidi ya taifa la Iran. ****
Na katika siku kama hii ya leo miaka 19 ilioyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliungana na kundi la nchi 10 zenye teknolojia ya kurusha chombo cha kupeleka angani satelaiti kilichopewa jina la Safire Omid kwa maana ya Balozi wa Matumaini. Operesheni hiyo ilifanyika kwa mafanikio.