Sep 18, 2026 03:58 UTC
  • Ijumaa, 18 Septemba, 2026

Leo ni Ijumaa tarehe 6 Mfunguo Saba Rabiuthani 1448 Hijria sawa na tarehe 18 Septemba mwaka 2026.

Katika siku kama ya leo miaka 1323 iliyopita, alifariki dunia Hisham Bin Abdul-Malik, kiongozi wa 10 katika silsila ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuwa madarakani kwa karibu kipindi cha miaka 20.

Hisham aliyekuwa mtawala dikteta, alizaliwa mwaka 72 Hijria na kushika uongozi wa Waislamu mwaka 105 Hijria. Hisham alikuwa mashuhuri kwa kuwa bahili, katili na dhalimu, ambaye aliwakandamiza Waislamu wa zama zake hususan wafuasi wa Ahlulbait wa Mtume (saw).

Mtawala huyo wa Bani Umayyah aliishi katika kipindi cha Imam Muhammad Baqir (as) mmoja wa wajukuu watukufu wa Nabii wa Muhammad (saw) na alimfanyia maudhi mengi mtukufu huyo na baadaye kutoa amri ya kuuawa kwake.

Mbali na hapo Hisham alifanya ukandamizaji mkubwa dhidi ya harakati ya Zaid bin Ali, mjukuu wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as). Baada ya kuuliwa Zaid, mtawala huyo dhalimu alitoa amri ya kuchomwa moto mwili wa mtukufu huyo.   

Licha kwamba katika kipindi cha utawala wa Bani Umayyah, Uislamu ulienea maeneo ya mashariki na magharibi mwa dunia, lakini kulishuhudiwa harakati kadhaa za Kiislamu za kupinga dhulma, kutokana na kushadidi dhulma na ukandamizaji wa Hisham bin Abdul-Malik, harakati ambazo zilipelekea kudhoofika kwa dola hilo la Bani Umayyah.   ****

Siku kama ya leo miaka 632 iliyopita alifariki dunia Mir Sayyid Sharif Gorgani, mtaalamu wa fasihi wa Iran huko Shiraz.

Gorgani alizaliwa mwaka 740 Hijiria karibu na mji wa Gorgani ya leo, kaskazini mwa nchi hii. Mir Sayyid Sharif Gorgani alihesabika kuwa msomi mkubwa katika zama hizo hususan katika uga wa elimu ya fasihi.

Ameacha athari mbalimbali mojawapo ikiwa ni kitabu kiitwacho "Risaalatul-Kubra fil-Mantwiq" na "Sharhul Mawaaqif."    ***

Siku kama ya leo miaka 596 iliyopita, sawa na tarehe sita Rabiuthani mwaka 852 Hijiria, alizaliwa Ibn Eyas, mwanahistoria mashuhuri wa Misri.

Ebn Iyas alinakili habari mbalimbali za kihistoria kwa mfumo wa nathari nyepesi, mfumo ambao ulikuwa hautumiwi na wanahistoria wengine. Mfumo huo ulikuwa na umuhimu mkubwa kwenye taaluma ya lugha ya Kiarabu.

Miongoni mwa athari muhimu ya kihistoria za Ibn Eyas ni pamoja na kitabu cha "Badaaiul-Zuhuur fii Waqaaiul-Duhuur" ambacho kinaelezea historia ya Misri tangu karne za nyuma hadi kipindi chake.

Aidha alifafanua maisha ya watawala wa Misri, ujenzi na uimarishwaji wake na mambo mbalimbali yaliyowahi kuikumba nchi hiyo katika karne za nyuma.   ***

Katika siku kama ya leo miaka 317 iliyopita, alizaliwa Samuel Johnson mwandishi wa drama, malenga na mwandishi wa visa wa Kiingereza.

Alianza shughuli zake za fasihi sambamba na ukosoaji wake katika taaluma hiyo. Baada ya muda mwanatamthilia huyo aliingia katika uga wa utunzi wa mashairi. Samuel Johnson aliaga dunia mwaka 1784. ***

Katika siku kama ya leo miaka 208 iliyopita, nchi ya Chile ilipata uhuru. Mwaka 1536 Chile ilidhibitiwa na Hispania. Sehemu kubwa ya kukoloniwa Chile, nchi hiyo ilikuwa sehemu ya utawala wa Naibu Mfalme wa Uhispania nchini Peru.    ****

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita yaani tarehe 18 Septemba 1947, Shirika la Ujasusi la Marekani CIA lilianzishwa.

CIA ni miongoni mwa mashirika ya kijasusi ya kutisha sana duniani, na lina jukumu la kukusanya na kuchambua taarifa kuhusu serikali za nchi za kigeni, makampuni na watu binafsi na kuripoti taarifa hizo kwa serikali ya Marekani.

Shirika hili lilichukua nafasi ya Idara ya Huduma za Kimkakati, ambayo iliundwa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ili kuratibu shughuli za kijasusi kati ya matawi mbalimbali ya jeshi la Merekani.  

Shirika la CIA, lenye idara na taasisi nyingi na pana, kama wakala wa ujasusi wa serikali ya Marekani, huwasaidia viongozi wa nchi hiyo katika kuingilia masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi ya nchi zingine.

Hadi sasa shirika hilo limehusika na mapinduzi ya serikali katika nchi mbalimbali zinazojitawala. Miongoni mwa mapinduzi hayo ni yale ya tarehe 28 Mordad 1332 Hijria Shamsia (19 Agosti 1953) nchini Iran kwa kushirikiana na shirika la ujasusi la Uingereza MI6.

Baada ya tukio la Septemba 11, 2001 lililoharibu majengo pacha (Twin Towers) huko New York, CIA ilipewa jukumu rasmi na la wazi la kuwateka nyara au kuwaua wapinzani wa Marekani duniani kote. ***

Na siku kama ya leo miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 27 Shahrivar mwaka 1367 Hijria Shamsia, aliaga dunia, Ustadh Muhammad Hussein Shahriyar mshairi mashuhuri wa Kiirani.

Alizaliwa mjini Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran na baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari katika Chuo cha Dar al-Funun mjini Tehran alijiunga na chuo cha tiba. Hata hivyo baada ya miaka michache aliacha masomo na kurejea katika kijiji alichozaliwa.

Ustadh Shahariyar alitoa mashairi yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 23. Sambamba na kushadidi harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini, Shahriyar aliungana na wimbi hilo kwa kutumia mashairi yake.

Vilevile alikuwa mashuhuri sana kwa kumpenda Mtume wa Ahlubaiti zake na mapenzi hayo yalidhihiri katika tungo na mashairi yake.