Kituo kisicho halali kinachohusishwa na ubalozi wa Ufaransa mjini Tehran chafungwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141592-kituo_kisicho_halali_kinachohusishwa_na_ubalozi_wa_ufaransa_mjini_tehran_chafungwa
Kituo kisicho halali kinachohusishwa na ubalozi wa Ufaransa, ambacho kilikuwa kikifanya shughuli zake kwa kisingizio cha kutoa mafunzo ya lugha, kimefungwa kwa amri ya Mwendesha Mashtaka wa Tehran.
(last modified 2026-09-20T13:40:41+00:00 )
Sep 20, 2026 13:39 UTC
  • Kituo kisicho halali kinachohusishwa na ubalozi wa Ufaransa mjini Tehran chafungwa
    Kituo kisicho halali kinachohusishwa na ubalozi wa Ufaransa mjini Tehran chafungwa

Kituo kisicho halali kinachohusishwa na ubalozi wa Ufaransa, ambacho kilikuwa kikifanya shughuli zake kwa kisingizio cha kutoa mafunzo ya lugha, kimefungwa kwa amri ya Mwendesha Mashtaka wa Tehran.


Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, kufuatia kuendelea shughuli na hatua zinazodaiwa kuwa kinyume cha sheria na kanuni za kidiplomasia zinazofanywa na Ufaransa, kituo kisicho halali kinachohusishwa na ubalozi wa Ufaransa mjini Tehran kimekuwa kikifanya shughuli zake kwa kisingizio cha kutoa mafunzo ya lugha za kigeni.

Licha ya kupewa maonyo mara kadhaa na taasisi za kisheria kuhusu umuhimu wa kupata kibali cha kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi, kituo hicho kilikataa kufanya hivyo na kivitendo, kikakiuka sheria za nchi.

Kwa msingi huo, na kwa amri ya mahakama iliyotolewa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Tehran, kituo hicho kinachohusishwa na ubalozi wa Ufaransa mjini Tehran, kinachojulikana kwa jina la CLF na ambacho kwa miaka kadhaa kimekuwa kikifanya shughuli zake chini ya mwavuli wa kufundisha lugha, kimefungwa.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, kituo hicho kilitumia vibaya shughuli za kufundisha lugha kama njia ya kutekeleza miradi inayokwenda kinyume na utamaduni wa Kiislamu na wa Iran, pamoja na kuhatarisha usalama wa taifa. Pia kituo hicho kinadaiwa kuwa kilijihusisha na kuwatambua watu wenye vipaji, kuunda mitandao miongoni mwao na kuwezesha wasomi hao kuondoka nchini.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, mwezi uliopita wa Agosti Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran iliwatimua wanadiplomasia wawili wa Ufaransa kutokana na mienendo yao haramu.