Jumatatu, 17 Agosti 2026
Leo ni Jumatatu 4 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1448 Hijria mwafaka na Agostu 17 2026.
Katika siku kama ya leo miaka 262 iliyopita alifariki dunia huko Karbala, Iraq faqihi, mpokezi wa Hadithi, mhakiki na mwandishi maarufu wa Kiislamu katika karne ya 12 Hijria, Sheikh Yusuf Bahrani.
Alijifunza elimu ya msingi kwa baba yake na baadaye alielekea Bahrain na Makka kwa ajili ya kupata elimu ya juu. Baadaye alielekea katika mji wa Fasa, kusini mwa Iran, ambako alianza kufundisha na kuandika vitabu. Wakati huo alianza kuandika kitabu chake kikubwa zaidi cha fiqhi kinachoitwa "al Hadaiqun Nadhirah".
Mwanzuoni huyo ameandika vitabu 32 katika taaluma mbalimbali vikiwemo "Anisul Musafir" na "Jalisul Khawatwir.'' ***
Miaka 81 iliyopita katika siku kama ya leo, wananchi wa Indonesia walianzisha mapambano ya kujikomboa kutoka katika makucha ya mkoloni Mholanzi.
Mapambano hayo yaliyoongozwa na Ahmad Sukarno yaliendelea kwa miaka minne huko Indonesia. Baada ya kushadidi mapambano hayo ya ukombozi ya wananchi Waislamu wa Indonesia, Umoja wa Mataifa uliiamuru serikali ya Uholanzi kuuasisi utawala kwa jina la " Umoja wa Indonesia na Uholanzi".
Jamhuri ya Indonesia ilivunja umoja huo mwaka 1956 na kutangaza uhuru wa nchi hiyo na Sukarno akawa Rais wa kwanza wa taifa hilo. ***
Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Gabon iliyoko magharibi mwa Afrika na katika pwani ya bahari ya Atlantic, ilipata uhuru. Wareno walifika huko Gabon kwa mara ya kwanza mwishoni mwa karne ya 15.
Hata hivyo nafasi ya kijiografia ya Gabon ilizuia kugunduliwa nchi hiyo hadi karne ya 19. Wafaransa waliwasili Gabon katikati ya karne ya 19 na kuidhinishwa kuitawala nchi hiyo katika mkutano uliofanyika huko Berlin, Ujerumani.
Hatimaye mwaka 1960 Gabon ilipata uhuru. Kijiografia nchi ya Gabon inapakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Congo, Cameroon na Guinea Bissau. ***
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, Rudolf Hess makamu wa dikteta wa zamani wa Ujerumani, Adolf Hitler, alijiua akiwa jela nchini Uingereza.
Hess ambaye alizaliwa mwaka 1894, alikuwa mmoja wa waasisi wa chama cha Kinazi na miongoni mwa viongozi wakuu wa serikali ya Hitler.
Rudolf Hess alihukumiwa kifungo cha maisha jela na mahakama ya jinai za kivita ya Nuremberg nchini Ujerumani baada ya nchi hiyo kushindwa katika Vita vya Pili vya Dunia. Hess alijiua akiwa jela mwaka 1987. ***
Katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, kundi la kwanza la mateka wa Kiirani waliokuwa wakishikiliwa katika magereza za kutisha za Saddam Hussein liliwasili katika ardhi ya Iran.
Kuachiwa huru mateka hao ilikuwa hatua muhimu ya kutekelezwa azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kati ya Iran na Iraq.
Saddam Hussein ambaye wakati huo alikuwa chini ya mashinikizo kutokana na kuivamia Kuwait alikubali kuwaachia huru mateka hao wa Iran na kurejea katika mipaka inayokubalika kimataifa ya nchi mbili baada ya kukubali mkataba wa mpaka wa Algeria. ****
Miaka 21 iliyopita katika siku kama ya leo wanajeshi wa utawala haramu wa Israel waliondoka kikamilifu kutoka katika eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina baada ya miaka 38 ya kukalia mabavu eneo hilo na kutenda jinai za kutisha.
Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, eneo la Ukanda wa Gaza limegeuka na kuwa nembo ya muqawama na kusimama kidete katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Wazayuni wakiwa na lengo la kushinda muqawama wa Kiislamu, wamelishambulia eneo la Gaza mara kadhaa ambapo shambulio la mwisho lilikuwa la mwaka 2014 vilivyodumu kwa muda wa siku 51.