Aug 13, 2026 02:53 UTC
  • Leo katika Historia
    Leo katika Historia

Leo ni Alkhamisi tarehe 29 Mfunguo Tano Safar 1448 Hijria sawa na tarehe 13 Agosti 2026.

Siku kama ya leo miaka 1244 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Ali bin Musa al Ridha AS, mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Mtukufu SAW.

Mtukufu huyo alizaliwa mwaka 148 Hijria katika mji wa Madina na alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Mussa al Kadhim AS. Mnamo mwaka 200 Hijria, Maamun, Khalifa wa Bani Abbasi, alimtaka Imam Ridha AS aelekee kwenye makao ya Khalifa huyo yaliyokuwa katika mji wa Marwi, kusini mashariki mwa Turkemenistan ambayo ilikuwa sehemu ya Khorasan Kuu.

Ijapokuwa kidhahiri Maamun alimfanya Imam Ridha kuwa mrithi wake, lakini kwa njia hiyo alikusudia kuimarisha zaidi nguvu za utawala wake. Utukufu na daraja ya juu ya kielimu na kiroho ya Imam Ridha na ushawishi wake uliokuwa ukiongezeka siku baada ya siku ndani ya fikra na nyoyo za watu vilimtia woga na hofu Maamun na hivyo akaamua kufanya njama za kumpa sumu na kumuua shahidi mjukuu huyo wa Mtume katika siku kama leo.

Imam AS amesema:"Mja bora zaidi ni yule ambaye kila anapofanya jema hufurahia, na kila anapokosea huomba msamaha, inapomfikia neema hushukuru, anapokumbana na masaibu husubiri, na wakati anapoghadhibika husamehe".    *****

Siku kama ya leo miaka 163 iliyopita aliaga dunia Frederick Eugene Delacroix, mchoraji maarufu wa Ufaransa. Eugene Delacroix alirithi kipaji cha sanaa ya uchoraji kutoka kwa mama yake.

Baada ya kupoteza wazazi wake wawili akiwa kijana mdogo na kujikuta akiishi maisha magumu sana ya umasikini, aliamua kufanya juhudi kubwa katika kujiendeleza na fani yake uchoraji.

Baadaye alianza kufanya maonyesho ya sanaa hiyo katika ukumbi wa jiji la Paris. Katika kipindi hicho baadhi ya watu walikuwa wakimfanyia maskhara na kumkebehi, hata hivyo hakuvunjika moyo na hatimaye kazi zake zilikuwa na taathira. Alipata umashuhuri katika kipindi kifupi na kazi zake zikapokewa sana katika jamii.   ***

Siku kama ya leo miaka 127, yaani tarehe 13 Agosti miaka 115 iliyopita, alizaliwa Alfred Hitchcock mtengeneza filamu mashuhuri wa Kiingereza.

Alionesha kazi yake ya kwanza mwaka 1920 na baadaye akaanza kujihusisha na uongozaji filamu. Filamu zake za kuogopesha na za kusisimua zilikuwa mashuhuri mno katika zama hizo. Filamu hizo zilimfanya awe mashuhuri kwa jina la the Master of Suspense.

Miongoni mwa filamu zake ni The Man Who Knew Too Much na Young and Innocent. Alfred Hitchcock aliaga dunia tarehe 28 Aprili 1980.   ***

Siku kama ya leo miaka 116 iliyopita, aliaga dunia Florence Nightingale, mwanzilishi wa uuguzi wa kisasa huko nchini Italia, akiwa na umri wa miaka 90.

Nightingale alizaliwa tarehe 12 Mei 1820 nchini Italia. Aliishi kipindi kirefu cha ujana wake nchini Uingereza. Akiwa kijana alifanya juhudi kubwa katika kuwasaidia watu, suala ambalo alilipa umuhimu mkubwa kuliko kitu kingine chochote na hatimaye alisabilia maisha yake kwa amjili ya kuuguza wagonjwa.

Bi, Florence Nightingale alikuwa muuguzi na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Alipewa lakabu ya ''Mwanamke Mwenye Taa Mkononi' kutokana na uvumilivu wake mkubwa na kujinyima usingizi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa nyakati za usiku. Alifanya juhudi kubwa pia kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali nyingi nchini Uingereza. Kazi hiyo aliyoifanya kwa miaka mingi bila kuchoka ilimdhoofisha sana kimwili kwa kadiri kwamba alikuwa kipofu mwishoni mwa umri wake na hatimaye aliaga dunia tarehe 13 Agosti 1910.    ***

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa.

Ilikuwa katikati ya karne ya 19 wakati nchi hiyo iliyokuwa ikijulikana hapo kabla kwa jina la Ubangi-Shari, ilipounganishwa na makoloni ya Ufaransa barani Afrika. Hata hivyo mwaka 1958, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilijipatia mamlaka ya ndani na miaka miwili baadaye yaani mwaka 1960, ikajikomboa na kupata uhuru kamili.   ***