Aug 16, 2026 03:32 UTC
  • Ijumaa Agosti 14 mwaka 2026

Leo ni Ijumaa tarehe Mosi Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1448 Hijria sawa na 14 Agosti mwaka 2026.

Siku kama ya leo miaka 1446 iliyopita, Mtume Muhammad SAW alianza Hijra yake ya kuhama Makka na kuelekea Madina, ikiwa imepita miaka 13 tokea alipobaathiwa na kupewa Utume.

Mtume wa Allah alihama Makka kutokana na kushadidi vitimbi vya washirikina wa mji huo ambao walikusudia kumdhuru na kumuua wakati wa usiku akiwa amelala nyumbani kwake. Imam Ali AS alijitolea mhanga, kwa kuamua kulala kwenye kitanda cha Mtume, ili maadui wasitambue kwamba Mtume wa Allah ameondoka mjini Makka.

Hijra ya Mtume SAW na matukio ya baada yake yalikuwa na umuhimu mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Uislamu kiasi kwamba lilitambuliwa kuwa mwanzo wa kalenda ya Kiislamu.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Mtume (saw) ndiye aliyekuwa wa kwanza kutumia hijra yake kama mwanzo wa kalenda ya Kiislamu kwani barua zote zilizoandikwa na mtukufu huyo kwa wakuu wa makabila na shakhsia maarufu alizisajili kwa kalenda hiyo.   ****

Tarehe Mosi Rabiul Awwal miaka 1381 iliyopita, ilianza harakati ya Tawwabin kwa lengo la kulipiza kisasi cha kuuawa shahidi Imam Hussein AS pamoja na wafuasi wake watiifu.

Awali, watu wa Kufa walimuomba Imam Hussein AS aelekee mjini humo kwa lengo la kuongoza harakati dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Yazid bin Muawiya lakini alizingirwa njiani na jeshi la mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya, na kuuawa shahidi.

Tawwabin ni kundi la watu wa Kufa ambalo lilijuta kwa kushindwa kutekeleza ahadi yake na kumuacha Imam Hussein na wafuasi wake wachache peke yao wapambane na majeshi ya Yazid. Kwa minajili hiyo watu hao walitubia makosa yao na kuamua kuanzisha harakati ya kulipiza kisasi wakiongozwa na Sulaiman bin Sorad dhidi ya jeshi la Yazid. Kundi hilo lilipigana kishujaa na jeshi la Yazid na wengi kati ya wapiganaji wake waliuawa shahidi.    ****

Tarehe 14 Agosti miaka 81 iliyopita yaani tarehe 14 Agosti mwaka 1945 Japan ilisalimu amri mbele ya vikosi vya Waitifaki.

Kwa utaratibu huo vita vilivyokuwa vimeanza mwaka 1939 kwa mashambulizi ya Ujerumani dhidi ya Poland vikafikia kikomo. Japan na Marekani ziliingia katika vita vikali Disemba mwaka 1941.

Vita hivyo vilimalizika baada ya Marekani kushambulia miji ya Hiroshima na Nagasaki kwa mabomu ya nyuklia ambayo yaliua karibu watu laki mbili. Kusalimu amri huko kwa Japan kwa hakika kulihitimisha Vita vya Pili vya Dunia.    *****

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, nchi ya Pakistan ilijitenga rasmi na India na kujitangazia uhuru wake.

Dini tukufu ya Kiislamu iliingia Bara Hindi katika karne ya 8 na sehemu ya ardhi hiyo ambayo leo inajulikana kwa jina la Pakistan ilikuwa mikononi mwa Waislamu hadi wakati ilipokaliwa kwa mabavu na Waingereza mwishoni mwa karne ya 18.

Chama cha Muslim League kikiongozwa na Muhammad Ali Jennah kilianzishwa mwaka 1906 kwa lengo la kuunda serikali ya Kiislamu baada ya kuanza harakati za wananchi wa India dhidi ya mkoloni Mwingereza. Chama hicho kilifanikiwa kuwashawishi Waislamu wa India na hatimaye kiliunda nchi ya Pakistan.     *****

Katika siku kama ya leo miaka miaka 70 iliyopita yaani tarehe 14 Agosti 1956, aliaga dunia malenga na mwandishi wa Kijerumani aliyejulikana kwa jina la Bertolt Brecht.

Brecht alizaliwa mwaka 1898 Miladia katika jimbo la Ugsbourg nchini Ujerumani. Malenga na mwandishi huyo wa Kijerumani alihitimu elimu ya juu katika taaluma ya sayansi asilia (bayolojia, kemia na fikikia). Malenga huyo wa Kijerumani ameacha vitabu na picha ambazo nyingi zinaeleza kuhusu utawala wa Manazi na udhalimu waliokuwa wakiutenda.    ****

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, Bahrain ilijitenga na ardhi ya Iran.

Kabla ya kudhihiri Uislamu, nchi hiyo ndogo iliyo katika Ghuba ya Uajemi ilikuwa katika utawala wa Iran na baada ya kubuniwa utawala wa Kiislamu ikawa inadhibitiwa na makhalifa wa Kiislamu.

Mwanzoni mwa karne ya 7 Hijiria kwa mara nyingine tena nchi hiyo iliunganishwa na Iran na baada ya hapo ikawa chini ya himaya ya Uingereza. Licha ya hayo Iran iliendelea kudai udhibiti na utawala wake kwa Bahrain na kulalamikia vikali hatua ya Uingereza ya kuitawala nchi hiyo.    *****

Na siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Agosti 2006, yalimalizika mapigano kati ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon na utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya kutolewa azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilikubaliwa na pande hizo mbili.

Mapigano hayo yaliyoanzishwa na utawala haramu wa Israel tarehe 12 Juni 2006, yalikuwa na lengo la kuidhoofisha na hata kuisambaratisha harakati ya Hizbullah. Kusimama kidete kwa wapiganaji wa Hizbullah dhidi ya majeshi ya Israel, kulimfanya Katibu Mkuu wake Sayyid Hassan Nasrullah apate uungaji mkono mkubwa katika ulimwengu wa Kiislamu.

Baada ya kukabiliwa na mapambano makali ya wapiganaji shupavu wa Hizbullah askari wa Kizayuni ambao awali walikataa mpango wa kusitisha vita walilazimika kuukubali mpango huo na kurudi nyuma bila ya mafanikio yoyote.   ****