Aug 16, 2026 03:26 UTC
  • Jumapili, 16 Agosti, 2026

Leo ni Jumapili 03 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1448 Hijria mwafaka 16 Agosti 2026 Miladia.

Siku kama leo miaka 138 iliyopita, alizaliwa Thomas Edward Lawrence, jasusi mkubwa wa Uingereza aliyekuwa na mchango mkubwa katika kuzidhoofisha nchi za Kiarabu. Kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia Lawrence, alikuwa amefanya safari katika nchi kadhaa za Kiarabu, ambapo sanjari na kujifunza lugha ya Kiarabu, alifahamu pia tamaduni na maisha ya Waarabu. Katika vita hivyo vya Kwanza vya Dunia vilivyojiri kati ya mwaka 1914 hadi 1918, na kwa msingi wa siasa za kikoloni za Uingereza, Lawrence alifanya njama kubwa kuyachochea makabila ya Kiarabu kwa kisingizio cha kutaka kujitawala, ili yaweze kujitenga mbali na utawala wa Othmania ambao katika vita hivyo ulikuwa ukikabiliana na Uingereza. Aidha Thomas Edward Lawrence alikuwa na nafasi pi aya kuuingiza madarakani ukoo wa Aal-Saud nchini Saudia, suala ambalo lilipelekea kupata umashuhuri mkubwa nchini Saudia.

***

Miaka 73 iliyopita katika siku kama ya leo, Muhammad Reza Pahlavi, mfalme wa mwisho wa Iran alikimbilia Italia akiwa pamoja na mkewe. Kabla ya kuikimbia Iran, Muhammad Reza Pahlavi alitia saini hukumu ya kuuzuliwa Waziri Mkuu, Muhammad Musaddiq, na alikimbia Italia baada ya kutambua kuwa, kulikuwepo mpango wa kufanyika mapinduzi dhidi yake. Wakati huo Musaddiq alikuwa ametaifisha sekta ya mafuta, suala ambalo lilihatarisha maslahi ya Uingereza nchini Iran. Siku tatu baadaye dola hilo la kikoloni lilitekeleza mapinduzi dhidi ya serikali ya Dokta Musaddiq na kumrejesha nchini dikteta na kibaraka wake, Shah Pahlavi ambaye aliitawala Iran hadi mwaka 1979 wakati Mapinduzi ya Kiislamu yaliyoongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini yalipopata ushindi na kuzika kabisa utawala wa kifalme hapa nchini.

***

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, kisiwa cha Cyprus kilipata uhuru baada ya machafuko ya miaka kadhaa. Kisiwa hicho ambacho hii leo kinaendeshwa chini ya mfumo wa jamhuri, kiko katika bahari ya Mediterraneanna kusini mwa Uturuki kikiwa na ukubwa wa zaidi ya kilomita mraba 9000. Kwa miaka kadhaa kisiwa cha Cyprus chenye historia kongwe na muhimu katika eneo kilikuwa chini ya falme za Iran, Ugiriki, Misri na utawala wa Othmania. Lakini mwaka 1878, utawala wa Othmania ulikabidhi usimamizi wa kisiwa hicho kwa Uingereza katika mkutano uliofanyika mjini Berlin Ujerumani na mwaka 1925 kisiwa cha Cyprus kikawa rasmi koloni la Uingereza.

***

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 25 Mordad 1372 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 16 Agosti mwaka 1993 alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzawari mwanachuoni mashuhuri wa nchini Iran. Ayatullah Sabzawari alizaliwa mnamo mwaka 1290 Hijiria Shamsia, sawa na mwaka 1911 Miladia, katika mji huo uliopo kaskazini mashariki mwa Iran. Mwanachuoni huyo licha ya kujipatia elimu zake za msingi katika mji wa Sabzawar na kisha kusoma elimu ya dini mjini Mash’had, alielekea Najaf nchin Iraq na kujipatia elimu ya juu ya maarifa ya Kiislamu. Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzawari ameandika vitabu tofauti maarufu zaidi ikiwa ni pamoja na vitabu vya ‘Mawaahibul-Rahman fii Tafsirul-Qur’an’ chenye juzuu 20, ‘Muhadh-Dhibul-Ahkaam fii Bayaanil-Halali wal-Haraam’ chenye juzuu 30 na ‘Tahdhibul-Usuulu’ chenye juzuu mbili.

***

Miaka 207 iliyopita katika siku kama ya leo Mauaji ya Peterloo (Peterloo Massacre) au mauaji ya wakulima wa Manchester yalitokea nchini Uingereza. Miaka minne baada ya kushindwa Napoleon, wakulima wapatao elfu sitini (60,000) kutoka Manchester, Uingereza, walikusanyika pamoja na familia zao katika eneo la shamba lililoitwa St Peter’s Field, ili kumsikiliza mkulima mpigania haki aliyeitwa Henry Hunt akitoa hotuba yake. Walikuwa wamekubaliana kwamba baada ya kusikiliza maneno ya Hunt, wangebaki hapo hapo na kufanya sherehe ya mapumziko ya pamoja (pikniki).  Hakimu wa mji huo alipatwa na wasiwasi baada ya kusikia habari za mkusanyiko huo. Kwa ombi la wamiliki wa ardhi (mabwanyenye), aliamua kuwatuma wapanda farasi wa kujitolea ili kumkamata Henry Hunt na kuvunja mkusanyiko huo. Wapanda farasi hao walipofika kwenye mkutano huo, Henry Hunt alikuwa akizungumza kuhusu mageuzi ya kilimo, ukusanyaji wa sahihi kwa ajili ya kuwasilisha ombi la kupitishwa sheria kuhusu suala hilo katika Bunge, pamoja na kufutwa Sheria ya Nafaka (Corn Laws). Askari hao wa farasi walivamia jukwaa ambalo Hunt alikuwa akihutubia na kuanza mapambano dhidi ya wakulima waliokuwa wamekusanyika kwa amani. Walifanya mauaji makubwa dhidi yao, licha ya kuwa mkutano huo haukuwa na silaha wala nia ya vurugu. Katika operesheni hiyo, jumla ya wanaume, wanawake na watoto 609 waliuawa au kujeruhiwa. Wanahistoria walitumia jina linalofanana na Waterloo — eneo ambako Napoleon alipigana vita yake ya mwisho na wapinzani wake — na tukio hili likapewa jina la “Mauaji ya Peterloo” (Peterloo Massacre) kama kumbukumbu ya ukatili uliotokea siku hiyo.

***