Wakenya watakiwa kutumia mitandao ya kijamii kuwaanika mafisadi
-
Felix Koskei
Mkuu wa Utumishi wa Umma nchini Kenya, Bw Felix Koskei, ametoa wito kwa Wakenya kushirikiana na serikali katika vita dhidi ya ufisadi ambao kwa miaka mingi umeathiri utoaji wa huduma za serikali.
Bw Koskei amesema kwamba licha ya hatua nyingi ambazo serikali ya Rais William Ruto imechukua kukabiliana na janga hilo, ufisadi bado umeenea katika ngazi za mashinani kote nchini.
Amesisitiza kuwa Wakenya wana uwezo mkubwa kupitia mitandao ya kijamii kurekodi na kufichua maafisa wala rushwa kwa kutumia simu zao.
“Serikali imejizatiti kung’oa ufisadi ili kuboresha huduma kwa umma. Serikali kupitia taasisi husika iko tayari kumshtaki kila mfisadi, lakini Wakenya lazima wasimame na kutumia nguvu ya mitandao ya kijamii kuwafichua wanaoendeleza ufisadi,” amesema Felix Koskei.
Alisema hayo katika Chuo Kikuu cha Cooperative jana Jumanne wakati wa uzinduzi wa warsha ya Kamati za Uangalizi wa Wananchi Dhidi ya Ufisadi za Kaunti (CACCOCs), zinazolenga kujumuisha wananchi katika vita dhidi ya ufisadi.
Kenya imekuwa ikisumbuliwa na ufisadi kwa miaka mingi na Wabunge amekuwa wakikashifiwa kwa kupokea mamilioni ya fedha ili kuwakingia kiifua maafisa wa umma wanaofika mbele ya kamati zao kuchunguzwa kuhusiana na tuhuma mbalimbali za ufisadi na uhalifu wa kifedha.
Vilevile, kumekuwa na madai ya wabunge kuhongwa ili kutupilia mbali ripoti ya kamati za Bunge zinazopendekeza maafisa wakuu wa serikali kuchukuliwa hatua za kisheria.