Netanyahu: Ni kweli tuliwaua kigaidi wanasayansi wa nyuklia wa Iran
(last modified Sun, 13 Jul 2025 06:57:25 GMT )
Jul 13, 2025 06:57 UTC
  • Netanyahu: Ni kweli tuliwaua kigaidi wanasayansi wa nyuklia wa Iran

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amekiri kwamba utawala huo wa Kizayuni uliwaua kwa utaratibu maalum wanasayansi wa nyuklia wa Iran.

Benjamin Netanyahu katika mahojiano na televisheni ya Marekani Fox News ameashiria mauaji ya hapo awali ya wanasayansi wa nyuklia wa Iran na kusema: "Tuliwalenga wanasayansi wa nyuklia wa Iran hapo awali, lakini hawalingani na wanasayansi mashuhuri waliouawa katika vita vya hivi karibuni."

Kukiri kwa Netanyahu juu ya mauaji hayo ya kigaidi kunathibitisha operesheni ya siri ya Israel inayolenga mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya kiraia, jambo ambalo wadadisi wa mambo wanasema linaongeza mivutano ya kikanda, na kuibua wasiwasi mkubwa wa kisheria na kimaadili.

Matamshi ya Netanyahu yamekuja katika hali ambayo, Katibu Mkuu wa Kamisheni ya Kitaifa ya Iran ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Hassan Fartousi amesema hujuma za Israel dhidi ya wanasayansi wa Iran ni tishio kwa "mantiki, sayansi na amani."

Katika mahojiano na Redio Monte Carlo ya Ufaransa jana Jumamosi, Dakta Fartousi alibainisha kuwa, wasomi na wanazuoni 32 wa Iran, ambao hawakuwa na uhusiano wowote na mpango wa nyuklia wa Iran, waliuawa na utawala wa Israel wakati wa vita vyake vya kichokozi dhidi ya nchi hii mwezi uliopita, jambo ambalo amelilaani na kulitaja kuwa ukiukaji wa sheria za kimataifa.