Raia wa US apigwa hadi kufa na walowezi wa Kizayuni Ukingo wa Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128238
Walowezi wa Israel wamempiga hadi kufa kijana mmoja raia wa Marekani katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu, kwa mujibu wa familia yake na mashirika ya kutetea haki za binadamu.
(last modified 2025-07-12T13:22:09+00:00 )
Jul 12, 2025 13:11 UTC
  • Raia wa US apigwa hadi kufa na walowezi wa Kizayuni Ukingo wa Magharibi

Walowezi wa Israel wamempiga hadi kufa kijana mmoja raia wa Marekani katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu, kwa mujibu wa familia yake na mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Wizara ya Afya ya Palestina imeripoti kuwa, Seif al-Din Muslat, raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 20 hivi kutoka Tampa, Florida, aliuawa siku ya Ijumaa katika mji wa Palestina wa Sinjil, kaskazini mwa Ramallah.

Wanafamilia wameliambia gazeti la The Washington Post kwamba, Muslat alipigwa hadi kufa na walowezi wa Kizayuni alipoenda kuwatembelea jamaa zake katika Ukingo wa Magharibi.

Binamu yake, Fatmah Muhammad, ameandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba, Muslat alisafiri kutoka Florida hadi Palestina kuona familia. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilithibitisha kuwa inafahamu ripoti hizo.

"Tunafahamu taarifa za kifo cha raia wa Marekani katika Ukingo wa Magharibi," msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa US aliiambia Reuters, akikataa kutoa maelezo zaidi kwa heshima ya familia ya mwathirika.

Mpalestina wa pili, aliyetambuliwa na Wizara ya Afya ya Palestina kama Mohammed Shalabi, alipigwa risasi na kufa wakati wa tukio hilo.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema walowezi wa Israel wameshadidisha hujuma za kinyama dhidi ya jamii za Wapalestina, mara nyingi chini ya ulinzi wa kijeshi.