Bunge la Waarabu lalaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Syria, Lebanon
Bunge la Waarabu limelaani vikali mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel dhidi ya maeneo ya Syria na Lebanon, na kutangaza kuwa huo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na tishio kubwa kwa utulivu wa kikanda.
Katika taarifa iliyotolewa jana Jumatano kwenye tovuti yake rasmi, Muungano wa Mabunge ya Nchi za Kiarabu umeshutumu mashambulizi hayo na kuyataja kama sehemu ya kampeni ya kimfumo ya kuyatwisha mataifa hayo kupitia nguvu za kijeshi.
Taarifa hiyo imesema hujuma hizo za Israel dhidi ya Syria na Lebanon zinaonyesha kutozingatia kabisa uhalali wa kimataifa na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Bunge la Waarabu limeonyesha mshikamano kamili na Syria na Lebanon katika kuhifadhi uhuru, mamlaka ya kujitawala eneo lao, na usalama wa raia wao. Kadhalika Bunge hilo la Waarabu limetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na madhubuti kukomesha uchokozi huo unaozidi kuongezeka.
Likirejelea msimamo wake usioyumba dhidi ya hatua zozote zinazohatarisha mamlaka ya mataifa ya Kiarabu, Bunge la Nchi za Kiarabu limesisitiza kwamba, usalama wa kudumu wa kieneo unategemea kuheshimiwa kamilifu sheria za kimataifa, mamlaka ya kitaifa ya nchi, na kutoingilia mambo yao ya ndani.
Haya yanajiri huku Israel ikishadidisha mashambulizi yake mapya dhidi ya Syria, ambapo mashambulizi ya punde zaidi yamelenga lango la makao makuu ya jeshi katika mji mkuu, Damascus. Vyombo vya habari vya Israel vimetaja mashambulizi hayo kuwa 'ujumbe' kwa kiongozi wa mpito wa Syria, Abu Mohammad al-Jolani.
Israel inadai kufanya hujuma hizo eti kuwaunga mkono watu wa jamii ya wachache wa Druze nchini Syria, ambao Tel Aviv inawaona kama waitifaki wake watarajiwa katika nchi hiyo ya Kiarabu iliyokumbwa na mgogoro. "Hatutaiacha (jamii ya) Druze ya Syria peke yake na tutatekeleza sera ya upokonyaji silaha."