Feb 01, 2026 02:24 UTC
  • Jumapili, Mosi Februari, 2026

Leo ni Jumapili 12 Shaaban 1447 Hijria mwafaka na Mosi Februari 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 949 iliyopita aliaga dunia Hassan bin Hafiz Andalusi, mpokezi wa Hadithi na tabibu mashuhuri wa Andalusia, sehemu ya Uhispania ya leo. Hassan bin Hafiz Andalusi aliyejuliikana kwa jina la Ghassani, alikuwa mwanafasihi mahiri na tabibu mweledi. Alikuwa na hati za kuvutia sana na kipaji kikubwa cha kutunga mashairi.  Kitabu cha 'Tamjiidul-Muhmal' ni miongoni mwa kazi za thamani za Hassan bin Hafiz al Andalusi na kinazungumzia na kufafanua maisha ya wapokezi wa Hadithi za Mtume (saw). 

Katika siku kama ya leo miaka 212 iliyopita, kulitokea vita vikali na vya umwagaji damu mkubwa maarufu kwa jina la Routier katika eneo lenye jina kama hilo karibu na Mto Ob kati ya jeshi lililokuwa na askari laki moja na 60 elfu la vikosi vya waitifaki wa nchi za Prussia, Austria na Sweden na jeshi lililokuwa na askari elfu 42 la Ufaransa chini ya uongozi wa Napoleon. Katika vita hivyo jeshi la Ufaransa lilishindwa vibaya na waitifaki kutokana na kutokuwa na moyo wa kupigana na uchache wa wapiganaji wake.  

Tarehe Mosi Februari miaka 68 iliyopita iliundwa Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu ya Syria na Misri. Baada ya kumalizika vita vya Suez na kurudi nyuma askari wa Uingereza, Ufaransa na utawala ghasibu wa Israel kutoka katika ardhi ya Misri, Gamal Abdul Nasser alitambuliwa kuwa kiongozi dhidi ya ukoloni wa Magharibi na dhidi ya Uzayuni katika ulimwengu wa Kiarabu na kupata umashuhuri mkubwa. Hatua ya kwanza ya kuanzisha muungano wa nchi za Kiarabu dhidi ya utawala haramu wa Israel na waungaji mkono wake wa Magharibi ilichukuliwa tarehe Mosi Februari 1958 baada ya Syria kutia saini makubaliano ya kuungana na Misri na muungano huo ulianza rasmi baada ya kura ya maamuzi ya tarehe 22 Februari 1958 katika nchi hizo mbili.

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita Imam Khomein (MA) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, alirejea nchini na kupokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi baada ya kuishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15. Mapokezi hayo makubwa ya wananchi wa Iran kwa Imam Khomeini hayajawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia ya sasa ya dunia. Baada ya kutoa hotuba fupi katika uwanja wa ndege wa Mehrabad, Imam Khomein alielekea moja kwa moja kwenye makaburi ya mashahidi waliouawa katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kutoa heshima kwa mashahidi hao ambako pia alitoa hotuba katika umati mkubwa wa wananchi. Kwa mara nyingine Imam aliitaja serikali ya Shapour Bakhtiar kuwa kibaraka wa Shah sanjari na kutangaza kuunda serikali mpya kwa msaada wa wananchi. Siku kumi baada ya kurejea nchini Imam, Mapinduzi ya Kiislamu yalipata ushindi kamili na kipindi hicho cha siku kumi za baina ya kurejea Imam nchini hadi kupata ushindi kamili Mapinduzi ya Kiislamu, kinajulikana hapa nchini kama "Alfajiri Kumi".

Katika siku kama ya leo miaka 13 iliyoita, Dakta Hassan Habibi mwanasiasa na mwanasheria wa Kiirani alifariki dunia. Alizaliwa mjini Tehran mwaka 1936. Hassan Habibi alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu (PhD) katika taaluma ya sosholojia na sheria katika Chuo Kikuu cha Sorbonne mjini Paris Ufaransa. Hassan Habibi aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali kama Waziri wa Miongozo na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Juu. Aidha alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran kuanzia mwaka 1989 hadi 2001 katika kipindi cha Urais wa Akbar Hashemi Rafsanjani na Sayyid Muhammad Khatami.

Tarehe Mosi Februari ni Siku ya Kimataifa ya Hijab. Siku ya Kimataifa ya Hijab huadhimishwa kila mwaka katika siku kama ya leo katika mataifa 140 duniani. Siku hii ilipendekezwa na kupasishwa kufuuatia ubunifu wa Nazma Khan mwamamke Muislamu Mbangladeshi-Mmarekani na baada ya radiamali za chuki dhidi ya Uislamu baada ya mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11. Moja ya malengo ya kuadhimisha siku hii ni kufikisha ujumbe kwa wanawake wa dunia kwamba, Hijab ya kiislamu sio kizuuzizi cha harakati za kijamii kwa wanawake. Lengo jingine ni kueneza utamaduni kwa ajili ya kusahihisha itikadi potofu katika mataifa ya Magharibi kuhusiana na vazi la mwanamke Muislamu.