Jumamosi, 8 Agosti, 2026
Leo ni Jumamosi 24 Mfunguo Tano Safar 1448 Hijria mwafaka 8 Agosti 2026 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 1063 iliyopita Sahib bin Abbad, mwanafasihi maarufu na msomi wa Kiislamu wa kizazi cha Dailami alifariki dunia. Sahib alikuwa mwandishi hodari na mtu mwenye hadhi na mashuhuri sana katika zama zake. Licha ya kwamba alikuwa waziri katika serikali ya kizazi cha Dailami, lakini alikuwa mtu mnyenyekevu na mwema kwa watu wa chini yake. Sahib bin Abbad ameandika vitabu vingi, na maarufu zaidi ni kile cha "al Muhiit" chenye juzuu saba.
***
Siku kama ya leo miaka 1373 iliyopita, vilitokea vita vya Ajnadeen katika eneo la Ajnadeen huko Palestina kati ya Waislamu na Warumi. Katika vita hivyo ambavyo havikuwa na mlingano hasa kwa kuzingatia kuwa, askari wa Kirumi walikuwa wengi mara kadhaa kuliko Waislamu, jeshi la Waislamu liliibuka na ushindi mkubwa kutokana na wapiganaji wake kuwa na irada na imani thabiti. Baada ya Warumi kushindwa vibaya na Waislamu waliamua kurejea nyuma hadi katika mpaka wa Palestina na Syria sambamba na kupoteza maeneo mengi yaliyokuwa chini ya udhibiti wao.
***
Siku kama ya leo miaka 2359 iliyopita sawa na tarehe 8 Agosti 333 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih AS, ilianza kazi ya ujenzi wa mji wa Alexandria nchini Misri, ambao leo hii unahesabiwa kuwa moja kati ya bandari muhimu kusini mwa Bahari ya Mediterranean. Ujenzi huo ulifanyika kwa amri ya Alexander Macedon huko kaskazini mwa Misri.
***
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Alhaj Sayyid Abul Qassim al Mussawi al Khoui, faqihi na marjaa mkubwa wa Kiislamu duniani, akiwa na umri wa miaka 96. Mwanachuoni huyo mashuhuri alizaliwa katika mji wa Khoui kaskazini magharibi mwa Iran na akiwa katika umri wa ubarobaro, alifuatana na baba yake mjini Najaf Iraq kwa ajili ya kujiendeleza kielimu. Katika zama za umarjaa wake, Ayatullahil Udhma al Khoui alitoa fatwa inayosisitiza udharura wa kuilinda Palestina na kuikomboa Quds kutoka mikononi mwa Wazayuni maghasibu. Alimu huyo mkubwa ameacha vitabu vingi vikiwemo 'Jawaahirul Usuul', 'Muntakhabu Rasaail', 'al Bayaan Fii Tafsiiril Qurani' na "Misbahul Faqaha".
***
Miaka 28 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 8 Agosti 1998, wanamgambo wa kundi la Taliban nchini Afghanistan waliuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa Mazar Sharif ulioko kaskazini mwa nchi hiyo. Baada ya kukaliwa kwa mabavu mji huo, wanamgambo wa Taleban waliushambulia ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji huo na kuwauwa shahidi wanadiplomasia 8 wa Kiirani na mwandishi mmoja wa habari. Kundi la Taliban liliasisiwa mwaka 1994 kwa ufadhili na usaidizi wa Marekani na Pakistan na kufanikiwa kuikalia sehemu kubwa ya ardhi ya Afghanistan.
***