Changamoto Mpya ya Marekani Kuhusu Iran: Kukimbia Vita au Makubaliano?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141050-changamoto_mpya_ya_marekani_kuhusu_iran_kukimbia_vita_au_makubaliano
Uchambuzi wa mwenendo na kauli za watawala wa Marekani unaonyesha kuwa Washington bado haijafikia uamuzi wa mwisho kuhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, huku ikiwa katika hali ya kutojua la kufanya kati ya kuendelea na vita au kufanya mazungumzo.
(last modified 2026-08-29T07:01:07+00:00 )
Aug 29, 2026 06:46 UTC
  • Changamoto Mpya ya Marekani Kuhusu Iran: Kukimbia Vita au Makubaliano?

Uchambuzi wa mwenendo na kauli za watawala wa Marekani unaonyesha kuwa Washington bado haijafikia uamuzi wa mwisho kuhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, huku ikiwa katika hali ya kutojua la kufanya kati ya kuendelea na vita au kufanya mazungumzo.

Miezi sita imepita tangu kuanza vita vya siku 40 kati ya Marekani na utawala wa Kizayuni kwa upande mmoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa upande wa pili. Ingawa pande hizo zilikubaliana kusitisha mapigano baada ya siku 40, lakini makubaliano hayo hayakudumu wala kumaliza kikamilifu mzozo uliopo, ambapo mapigano ya hapa na pale yameendelea kuripotiwa mara kadhaa kati ya pande hizo. Sasa, kukiwa hakuna dalili zozote za kuelekea kwenye makubaliano, Marekani, kupitia hatua ambayo Waziri wake wa Fedha ameielezea kama "mbano wa kiuchumi", inajaribu kusababisha mzozo wa kiuchumi ndani ya Iran ili iweze kuilazimisha iketi kwenye meza ya mazungumzo na hatimaye kuitwisha matakwa yake, au kuanzisha vita vipya dhidi ya nchi hii.

Swali muhimu ni je, kwa nini Marekani inaendelea kutarajia kuwa chaguo la vita litakuwa na matokeo chanya? Jibu la msingi kuhusiana na suala hili ni kuporomoka kwa itibari ya Marekani duniani. Fareed Zakaria, mchambuzi mashuhuri wa Marekani, aliandika hivi karibuni kwamba: "Suala la vita dhidi ya Iran limekuwa mfano wa wazi kabisa wa namna hadhi na itibari ya taifa kubwa duniani vinavyoweza kuharibiwa." Marekani, ambayo hujiona kuwa taifa lenye nguvu kuu na linalotawala mfumo wa kimataifa, imeshindwa kufikia malengo yake makuu dhidi ya Iran kwa kutumia njia za kijeshi. Kwa hakika, wananadharia mashuhuri wa Marekani kama vile John Mearsheimer wanasema waziwazi kuwa Marekani imeshindwa katika vita vyake vya kichokozi dhidi ya Iran. Mbali na hayo, hadi sasa Marekani imeshindwa hata kuiburuza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenye meza ya mazungumzo au kuitwisha matakwa yake kupitia mashinikizo ya kiuchumi.

Scott Ritter, afisa wa zamani wa Marekani na mkaguzi wa silaha wa Umoja wa Mataifa, anasema: "Leo hii, hakuna mtu yeyote duniani anayeamini kuwa Marekani imeshinda vita hivi, wala kuwa na uwezo wa kutekeleza mashinikizo yoyote makubwa ya kiuchumi. Mawazo haya ni ya kufikirika tu na yanapatikana tu katika ulimwengu wa ndoto za Donald Trump." Katika mazingira haya, Trump na timu yake wanatarajia kupata ushindi dhidi ya Iran kupitia vita vipya, wazo ambalo linatazamwa kwa mashaka makubwa, na hata Wamarekani wenyewe. Hivyo, hakuna makubaliano ndani ya mfumo wa madaraka wa Marekani kuhusu kuanzishwa vita vipya dhidi ya Iran, bali wengine wanaona hatua hiyo kuwa kinyume na maslahi ya Marekani.

Swali jingine linajitokeza hapa nalo ni kuwa je, kwa nini Marekani haifanyi makubaliano ya kweli na Iran? Kiuhalisia, ingawa serikali ya Marekani haifutilii mbali uwezekano wa kuendelea kufanya mazungumzo na Iran, lakini wakati huo huo haifuatilii kwa nia njema kufikia makubaliano halisi na Tehran. Sababu kuu ya jambo hili ni kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakataa kukubaliana na madai ya Marekani yasiyo halali wala kuwa na mantiki, kama vile kusitisha kabisa urutubishaji wa urani, kupeleka nje akiba yake ya urani iliyorutubishwa au kurejesha hali ya Lango-Bahari la Hormuz katika hali ya kabla ya vita vya siku 40. Kwa maneno mengine, Marekani inajaribu kuitwisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran matakwa yake ya kidhalimu kupitia mazungumzo, huku Tehran ikionyesha wazi kuwa haitakubaliana na matakwa hayo yasiyo na mantiki. Hivyo, watawala wa sasa wa Marekani wanaamini kuwa kufanya mazungumzo na Iran katika mazingira haya kutapelekea kutolewa fursa nyingi za Marekani kwa Tehran.

Huku Marekani ikiwa imekwama katika njia panda, ikiyumbayumba kati ya kurejea vitani au kufikia makubaliano na Iran, imeamua kutoa kipaumbele kwa juhudi za kuongeza mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya nchi hii. Pamoja na hayo, lakini la muhimu ni kwamba, Iran inayachukulia mashinikizo haya ya kiuchumi kuwa sawa na hatua ya kijeshi, na kuonya kuwa iwapo yataendelea, itabadilisha mkakati wake wa kukabiliana na Marekani kutoka wa kujihami kijeshi hadi wa kuanzisha mashambulii ili kutetea maslahi yake ya kitaifa. Onyo hili pia linaashiria kuwa tishio na majigambo ya muda mrefu ya Marekani dhidi ya Iran, kwamba "machaguo yote yapo mezani", yamepoteza nguvu zake, na kwamba Iran haiogopi tena vita na Marekani na kuwa iko tayari kuanzisha mashambuli ya kijeshi wakati wowote dhidi ya nchi hiyo ya kibeberu, kwa ajili ya kulinda maslahi yake ya kitaifa.