Umoja wa Afrika: Mapigano yanaendelea DRC licha ya makubaliano ya amani
-
Umoja wa Afrika: Mapigano yanaendelea DRC licha ya makubaliano ya amani
Umoja wa Afrika (AU) umetangaza kuwa, mapigano yanaendelea kushuhudiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo licha ya makubaliano yaliyosainiwa na michakato ya amani inayoendelea.
Hayo yameelezwa na Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye ambaye pia ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika (AU).
"Nchini DRC, mapigano yanaendelea licha ya makubaliano mbalimbali kusainiwa na michakato ya amani inayoendelea," Rais Ndayishimiye alisema wakati wa ufunguzi wa kikao cha dharura cha 21 cha Umoja wa Afrika, kuhusu kuimarisha mifumo ya kuzuia na kutatua migogoro barani Afrika kilichofanyika mjini Luanda Angola.
Mwenyekiti huyo wa Umoja wa Afrika aliiweka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo miongoni mwa migogoro inayolazimisha Umoja wa Afrika kuchukua hatua katika pande mbili: kuzuia kuzuka kwa migogoro mipya na kujaribu kutatua ile ambayo tayari inaendelea. Pia alivitaja vita nchini Sudan na vurugu ba machafuko mkatika eneo la Sahel Afrika.
Kulingana na Evariste Ndayishimiye, Afrika haikosi vyombo vya utendaji. Ina Baraza la Amani na Usalama, Mfumo wa Bara wa Onyo la Mapema, Jopo la Wazee, Kikosi cha Akiba cha Afrika, na Mfuko wa Amani.
Lakini alieleza masikitiko yake kwamba, hatua bado huchukuliwa mara nyingi pale ambapo hali tayari imekaribia kuwa mbaya na isiyodhibitika. Kiongozi huyo wa Umoja wa Afrika ametoa wito wa kubadilisha tahadhari za mapema kuwa majibu ya haraka na kuimarisha uzuiaji, upatanishi na diplomasia ya kuzuia migogoro.
Évariste Ndayishimiye pia aliona kuwa utatuzi wa migogoro hauwezi kuishia tu kwenye mazungumzo na utiaji saini wa makubaliano. Lazima pia ushughulikie vyanzo vya msingi vya ghasia, miongoni mwa hivyo alitaja utawala mbaya, udhaifu wa taasisi, ubaguzi wa kisiasa, ukosefu wa usawa, dhulma ya kijamii na ukosefu wa fursa kwa vijana.