Aug 29, 2026 06:01 UTC
  • Jumamosi, 29 Agosti, 2026

Leo ni Jumamosi, 16 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1448 Hijria mwafaka 29 Agosti 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1447 kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Swala ya kwanza ya Ijumaa iliswaliwa na Mtume Muhammad (saw) baada ya mtukufu huyo kuhama mji wa Makka. Baada ya kuwasili katika eneo la Bani Salim bin Auf kwa jina la Quba karibu na Madina wakati wa adhuhuri, Mtume (saw) alitoa hotuba na kusimamisha Swala ya Ijumaa mahala hapo. Wanahistoria wanasema hiyo ilikuwa Swala ya kwanza ya Ijumaa katika Uislamu. Hatua hiyo pia inaonesha umuhimu wa ibada hiyo ya kiroho na kisiasa ambayo Bwana Mtume aliamua kuitekeleza mara tu baada ya kuwasili karibu na mji wa Madina. Baadaye Waislamu walijenga msikiti katika eneo hilo palipofanyika Swala ya Ijumaa ya kwanza katika Uislamu.

***

Miaka 164 iliyopita, katika siku kama ya leo, tarehe 29 Agosti 1862, Maurice Maeterlinck, mwandishi mashuhuri wa Ubelgiji, alizaliwa katika jiji la Ghent, Ubelgiji. Baada ya kumaliza masomo yake, alikwenda Paris, ambako alikutana na wasomi na watu mashuhuri katika ulimwengu wa fasihi, ambao waliamini kwamba ushairi unapaswa kuwa tafsiri ya hisia na mihemko inayochanua kutoka ndani kabisa ya nafsi ya mwanadamu. Katika safari hiyo ndipo Maeterlinck alipoanza kuiwasilisha kazi zake bora na mashuhuri kwa ulimwengu wa fasihi. Mwaka 1911, alitunukiwa Tuzo ya Nobel ya Fasihi. Baada ya kuanza kwa Vita vya Pili vya Dunia, Maeterlinck alikimbilia Marekani, ambako aliishi hadi mwisho wa maisha yake. Baadaye alifanya maendeleo makubwa katika taaluma ya uandishi wa tamthilia, kiasi kwamba alipewa jina la “Shakespeare wa Ubelgiji.”

***

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita Urusi ya zamani ilifanya majaribio ya siri ya bomu lake la kwanza la nyuklia. Kwa utaratibu huo Urusi ikawa nchi ya pili yenye mabomu ya nyuklia baada ya Marekani suala ambalo liliibua mlingano wa nguvu kati ya nchi hizo mbili ambao ulipewa jina la “Mlingano wa Hofu.” Kwani katika hali hiyo kila mmoja wao aliogopa kutumia silaha hizo za nyuklia dhidi ya mwenzake kwa kuogopa kushambuliwa pia na silaha kama hizo. Tangu wakati huo Marekani na Urusi ya zamani ziliingia katika vita vya kipropaganda. Vita hivyo vilipewa jina la "Vita Baridi" au Cold War kwa kimombo. Vita hivyo vya kati ya kambi ya Mashariki na Magharibi viliendelea hadi wakati wa kusambaratika Urusi ya zamani mwaka 1991.

***

Miaka 58 iliyopita katika siku kama ya leo ya 7 Shahrivar 1348 Hijria Shamsia, Seyyed Zia al-Din Tabatabaei», mwanasiasa kibaraka wa Iran alifariki dunia. Seyyed Zia al-Din Tabatabaei alizaliwa mwaka 1268 kwa kalenda ya Shamsia mjini Shiraz, kusini mwa Iran. Alisomea elimu za kisasa pamoja na kwa kiwango fulani masomo ya dini. Aidha, aliweza kujifunza lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kirusi. Wakati wa Mapinduzi ya Katiba (Constitutional Revolution) nchini Iran, alijionyesha kuwa mmoja wa wafuasi wa harakati hiyo na alianzisha magazeti kadhaa, ambayo kila moja lilifungwa kwa sababu mbalimbali. Mwelekeo wa kisiasa wa Seyyed Zia al-Din Tabatabaei, ambao aliendelea nao hadi mwisho wa maisha yake, ulikuwa kuunga mkono sera za kikoloni za Uingereza nchini Iran. Kwa sababu hiyo, katika mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa kwa msaada wa Uingereza mwaka 1299 Shamsia, alishirikiana na Reza Khan na akawa na nafasi kubwa katika tukio hilo. Baadaye, Ahmad Shah, mfalme wa mwisho wa ukoo wa Qajar, alimteua kuwa Waziri Mkuu wa Iran. Hata hivyo, sera zake zilizoshindwa pamoja na ushindani wake wa kisiasa na Reza Khan vilisababisha kuondolewa kwake madarakani baada ya miezi mitatu tu. Licha ya kuondolewa madarakani, katika kipindi chote cha historia ya kisiasa ya utawala wa Pahlavi, Tabatabaei aliendelea kutajwa kama mtu aliyekuwa akiaminiwa na Uingereza.

***

Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, msanii na mchoraji maarufu wa katuni wa Palestina, Naji al Ali, ambaye alikuwa ameshambuliwa na maajenti wa Shirika la Ujasusi la Israel MOSSAD huko London, Uingereza alifariki dunia baada ya siku 38 za kuwa katika hali ya kupoteza fahamu. Al-Ali alizaliwa mwaka 1937 huko Palestina na alilazimika kukimbia nchi yake akiwa bado mtoto akiwa pamoja na familia yake na kuishi katika kambi ya wakimbizi ya Ain al-Halwa kusini mwa Lebanon kutokana na ukatili na unyama wa Wazayuni. Alishuhudia kwa karibu mashaka na masaibu ya Wapalestina na akaamua kutumia kipawa chake cha usanii kufichua unyama na ukatili wa utawala ghasibu wa Israel kwa kutumia sanaa ya uchoraji vibonzo. Hatimaye magaidi wa Shirika la Ujasusi la Israel MOSSAD walimshambulia na kumuua mwanamapambano huyo akiwa njiani kuelekea ofisini kwake mjini London. Miezi sita baada ya kufariki kwake dunia Jumuiya ya Kimataifa ya Wachapishaji ilimtunuku msanii huyo tuzo ya Kalamu ya Dhahabu ya Uhuru. 

***

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Shahrivar 1369 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sayyid Shahabuddin Mar'ashi Najafi mmoja wa Marajii na viongozi wa juu wa Kiislamu hapa nchini, akiwa na umri wa miaka 96. Alimu huyo alisoma elimu za fiqihi, Usul Fiqihi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani, teolojia na misingi ya kimaadili katika vyuo vikuu vya kidini katika miji ya Kadhmein na Najaf Iraq. Moja ya athari kubwa zilizoachwa na Ayatullah Mar'ashi Najafi ni maktaba kubwa ya vitabu iliyoko katika mji wa Qum, ambayo inahesabiwa kuwa ya aina yake duniani. 

***