Jan 10, 2026 02:28 UTC
  • Jumamosi, 10 Januari, 2026

Leo ni Jumamosi 20 Rajab 1447 Hijria mwafaka na 10 Januari 2026 Miladia.

Miaka 1434 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vilitokea vita vya Yarmuk kati ya jeshi la Kiislamu na jeshi la utawala wa kifalme wa Roma ya Mashariki katika bonde lililojulikana kwa jina hilo huko Palestina. Ushindi wa Waislamu huko Sham, yaani Syria ya sasa ulimpelekea mfalme wa Roma kuandaa jeshi kubwa kwa ajili ya kupigana na Waislamu. Lakini, Waislamu waliweza kutoa pigo kwa wanajeshi wa mfalme wa Roma licha ya kuwa na idadi ndogo ya wapiganaji na suhula chache za kivita. Kufuatia ushindi huo Waislamu walisonga mbele na kufika eneo la Mashariki la Ufalme wa Roma na mwaka mmoja baada ya hapo jeshi la Kiislamu lilifanikiwa kuchukua udhibiti wa mji wa Baitul Muqaddas pasina umwagaji damu.  ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 174 iliyopita, Mirza Taqi Khan Amir Kabir, mwanasiasa na kansela mwenye ustahiki wa kipindi cha utawala wa Qajar nchini Iran aliuawa kwa amri ya Nassir al-Din Shah. Kutokana na kuonyesha uwezo na kipaji, alifanikiwa kuchukua wadhifa wa kansela katika zama za utawala wa Nasser al-Din Shah Qajar. Amir Kabir alikuwa mtu asiyekubali kuburuzwa, mwenye imani na mzalendo, msomi na mpenda utamaduni. Hakuwa na woga wowote katika njia ya kuhudumia wananchi wa Iran na katika kipindi chake kifupi cha ukansela  alifanya huduma kubwa kwa wananchi sambamba na mageuzi mengi kwa maslahi ya wananchi. Amir Kabir alifanya juhudi kubwa kuzuia uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya Iran na uporaji wa mali za umma uliokuwa ukifanywa na mabwanyenye. Miongoni mwa mageuzi aliofanya ni kuanzisha shule ya Darul-Funun, kutarjumu na kuchapisha vitabu. Misimamo na hatua zake ambazo zilikuwa dhidi ya maslahi ya madola ya kigeni, ziliibua chuki za madola hayo. Hatimaye kufuatia mashinikizo ya nje na mamluki wa ndani, Shah Qajar alimuuzulu wadhifa wake na kumbaidishia katika mji wa Kashan na kisha kuuawa katika siku kama ya leo.

 

Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita, inayosadifiana na 10 Januari 1920, Jumuiya ya Mataifa ilianza shughuli zake rasmi huko Geneva, Uswisi. Jumuiya hiyo iliundwa baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia kwa shabaha ya kuimarisha amani na usalama duniani. Mwanzoni nchi za Kiafrika na Urusi hazikujiunga na jumuiya hiyo na badala yake nchi za Uingereza na Ufaransa ndizo zilizobeba jukumu la kuzisaidia nchi hizo. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, mnamo mwezi Aprili 1946, uliundwa Umoja wa Mataifa na kuchukua nafasi ya Jumuiya ya Mataifa, ingawa matatizo yaliyokuwa yakiikumba Jumuiya ya Mataifa bado yanaendelea kuukumba Umoja wa Mataifa hadi hii leo.

 

Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, wataalamu wawili wa Uswisi walifanikiwa kutengeneza saa ya elekroniki. Baada ya miaka 12 ya juhudi kubwa, hatimaye wataalamu Solvil na Titus walifanikiwa kutengeneza chombo hicho kwa kuweka vifaa kadhaa muhimu na makini. Aina hii ya saa ni makini mno na hufanya makosa machache sana ikilinganishwa na saa nyingine. 

 

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, jaribio la mauaji dhidi ya ya Hujjatul Islam Seyyed Mohammad Khamenei, mwakilishi wa Majlisi ya Ushauri (bunge la Iran) lilifeli. Sambamba na kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu na mwanzo wa njama za ndani za kuwaondoa watu mashuhuri wa mapinduzi katika medani ya shughuli za nchi, vikundi vya upinzani wa mfumo vilifanya njama za kuwaondoa watu hawa. Mwaka wa 1360 Hijria ni moja wa miaka ambayo watu mashuhuri waliuawa na wengi wao walipata neema ya kuuawa kishahidi. Katika moja ya mauaji haya ya Munafiqin, Hujjatul Islam Seyyed Mohammad Khamenei, kaka wa Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, akiwa mwakilishi wa watu wa Mashhad katika Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu ya Iran, alishambuliwa na wanachama wa Kundi la Munafiqi alipokuwa akielekea Bungeli. Alijeruhiwa kiunoni katika tukio hilo huku walinzi wake wawili wakiuawa kishahidi.