Je, ni malengo gani yanafuatiliwa na Marekani katika kushambulia miundombinu ya Iran?
Kwa madai ya kushambuliwa meli kadhaa zinazopita kinyume cha sheria kusini mwa Lango-Bahari la Hormuz na kukiukwa Mkataba wa Islamabad, Rais Donald Trump wa Marekani aliamuru kuanzishwa tena mashambulizi ya kichokozi dhidi ya Iran kuanzia Julai 7, ambapo pia mzingiro wa majini dhidi ya Iran ulirejeshwa mnamo Julai 14.
Trump alitangaza kando ya mkutano wa NATO mjini Ankara kwamba hakuna tena maelewano yaliyopo kati ya Marekani na Iran na kwamba usitishaji vita umemalizika. Kufuatia kurejea kwa uchokozi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran, na hatua za kujilinda za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kushambulia kambi za Marekani zinazotumika kama vituo vya kuendeleza mashambulizi hayo, macho ya dunia kwa mara nyingine tena yameelekezwa kwenye Lango Bahari la Hormuz kama kitovu cha mzozo mpya kati ya Iran na Marekani.
Katika mfululizo wa hivi karibuni wa mashambulizi, Marekani imeshambulia kigaidi maeneo mbalimbali katika ardhi ya kusini mwa Iran. Ingawa awali Washington ilidai kuwa ilikuwa inashambulia maeneo ya kijeshi tu, kama vituo vya rada na mawasiliano, mifumo ya makombora ya ulinzi wa pwani, na vifaa vya majini, ikiwa ni katika jitihada zake za eti kuizuia Iran isivuruge usafiri katika Lango la Hormuz, mashambulizi ya hivi karibuni yamelenga waziwazi miundombinu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na madaraja na mitambo ya maji na nishati. Inaonekana kuwa lengo hasa la Marekani kushambulia miundombinu ya Iran ni mkakati mkubwa unaotekelezwa katika hatua tofauti kwa ajili ya kufikia lengo kuu la kubadilisha uwiano wa nguvu katika eneo, hasa kuhusiana na Lango-Bahari la Hormuz, kwa maslahi ya Marekani na utawala haramu wa Israel.
Lengo kuu lililotangazwa hadharani na Marekani ni kuvunja uwezo wa kijeshi wa Iran, hasa ule wa Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ili eti kulinda usalama wa usafiri wa meli katika Lango-Bahari la Hormuz. Kampeni hii, iliyoanzishwa tarehe 7 Julai katika kujibu mashambulizi ya Iran dhidi ya meli za kibiashara zinazokiuka sheria katika lango hilo, imelenga vituo vya pwani, mifumo ya rada na makombora, pamoja na maghala ya silaha yaliyoko chini ya ardhi. Kuelekezwa mashambulizi ya adui katika Mkoa wa Hormozgan na Bandar Abbas, ikifuatiwa na mikoa ya Bushehr, Khuzestan, pamoja na Sistan na Baluchestan, kunadhihirisha lengo kuu la Washington la kudhoofisha uwezo wa Iran wa kutumia nguvu zake za kijeshi katika Lango-Bahari la Hormuz.
Katika hatua inayofuata, Marekani inalenga kudhoofisha pakubwa uwezo wa Iran wa usafirishaji na usambazaji wa rasilimali kwa kulenga miundombinu muhimu inayosaidia shughuli za kijeshi. Mashambulizi dhidi ya madaraja, vituo vya reli, na barabara kusini mwa Iran yanalenga kukata njia za usambazaji bidhaa na zana hasa zile zinazoelekea Bandar Abbas, na hivyo kuzuia usafirishaji wa wanajeshi na vifaa vya kijeshi kelekea maeneo ya pwani. Mkakati huu unaashiria mabadiliko katika mbinu za kijeshi za Marekani, kutoka hatua za kujibu mashambulizi hadi hatua za kimfumo na za muda mrefu, zilizobuniwa kwa ajili ya kudhoofisha misingi ya uwezo wa Iran wa kutekeleza operesheni za kijeshi.
Mashambulizi kwenye miundombinu, kama vile mitambo ya kuzalisha umeme na mifumo ya maji safi ya kunywa yanavuka mipaka ya malengo ya kijeshi. Yanatumika kama njia ya kuongeza mashinikizo ya kiuchumi na kisiasa dhidi ya Iran na kuzidisha mzigo kwa wananchi wa Iran. Mashambulizi haya haramu, ambayo awali Trump alitishia kuyaanzisha, yanatoa ujumbe wa wazi: Iwapo Iran haitarejea kwenye meza ya mazungumzo, ili kukubali matakwa ya Washington bila masharti, gharama watakayolipa wananchi wa Iran itakuwa kubwa na ngumu zaidi. Kwa kuongeza mashinikizo hayo, Marekani inalenga kuilazimisha Iran itie saini makubaliano yanayoendana na matakwa yake yenyewe.
Wataalamu wanaona kuwa lengo kuu la mashambulizi haya linavuka mipaka ya malengo yaliyotangazwa hadharani. Baadhi wanayachukulia kama utangulizi wa operesheni ya nchi kavu inayoweza kufanyika kusini mwa Iran, kwa lengo la kuhakikisha Marekani inadhibiti Lango-Bahari la Hormuz. Aidha, mashambulizi haya yanaipa Marekani chaguzi kadhaa za kijeshi na yanaweza kufungua njia ya kuchukuliwa hatua kubwa zaidi, kama vile kushambulia sekta ya nishati ya Iran.
Hatimaye, matokeo ya jumla ya mashambulizi haya yanaashiria kampeni iliyoanzishwa kwa ajili ya kubadilisha kimsingi uwiano wa nguvu katika eneo, ikilenga kudhibiti Lango-Bahari la Hormuz na hivyo kuiwekea Iran mashinikizo makubwa zaidi.