Jul 20, 2026 05:45 UTC
  • Jumatatu tarehe 20 Julai 2026

Leo ni tarehe 5 Safar 1448 hijria sawa na tarehe 20 Julai mwaka 2026.

Siku kama ya leo miaka 1387 iliyopita Ruqayyah binti mdogo wa Imam Hussein bin Ali (as) alikufa shahidi akiwa huko Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyya.

Ruqayyah ambaye pia anajulikana kwa jina la Fatima binti Hussein (as) alikuwa binti wa mwisho wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) kutoka kwa mkewe, Ummu Is’haq binti Twalha.

Wanahistoria wanasema mtoto huyo alikuwa na umri wa miaka 3, 4 au 7. Mtoto huyo alikuwa akimpenda sana Imam Hussein na aliandamana naye pamoja na familia yake katika medani ya Karbala.

Baada ya kuuawa shahidi baba yake, ndugu na masahaba wa Imam, Ruqayya alikamatwa mateka na askari wa Yazid akiwa pamoja na watu wengine wa Nyumba ya Mtume na kupelekwa Sham. Huko alikuwa akilia mchana usiku. Wahistoria wanasema mtawala Yazidi aliamuru kichwa cha Imam Hussein kipelekwe na kutupwa mbele ya binti huyo mdogo ambaye alilia na kuzimia kisha akakata roho.     ****

Miaka 216 iliyopita katika siku kama ya leo, uhuru wa Colombia ulitangazwa rasmi. Colombia iligunduliwa mwishoni mwa karne ya 15 na Wahispania na kuanza kukoloniwa.

Kuanzia mwishoni mwa karne ya 18, harakati za kupigania uhuru za wananchi wa nchi hiyo ziliongezeka na hatimaye harakati hizo kuzaa matunda katika siku kama ya leo. Hatua ya Napoleon Bonaparte ya kuikalia kwa mabavu Uhispania, ilizipatia fursa nzuri nchi makoloni ya Uhispania ikiwemo Colombia kuzidisha mapambano ya ukombozi.   ***

Katika siku kama ya leo miaka 160 iliyopita, Georg Friedrich Bernhard Riemann, mwanahisabati wa Kijerumani aliaga dunia baada ya kuugua maradhi ya kifua kikuu.

Georg Friedrich alizaliwa mwaka 1826 katika mji wa Hanover nchini Ujerumani na baada ya kumaliza masomo yake ya awali aliendelea na masomo ya hisabati. Alipofikisha umri wa miaka 28 Bernard Riemann alikuwa tayari ni mhadhiri wa Chuo Kikuu katika uwanja huo wa hisabati. ***

Miaka 89 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Guglielmo Marconi mvumbuzi wa radio wa Kiitalia akiwa na umri wa miaka 63.

Guglielmo alizaliwa mwaka 1874 huku akiwa mtoto wa mfanyabiashara mmoja wa Kiitalia.

Marconi alipenda sana kujifunza masuala ya ufundi na sanaa tangu akiwa kijana mdogo ambapo alianza utafiti wa mawimbi ya sauti. Marconi hatimaye alifanikiwa kuvumbua radio baada ya utafiti wake huo na baadaye akaikamilisha bila ya kutumia waya.    ****

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika mwezini.

Katika siku hiyo wanaanga wa Kimarekani Neil Armstrong na Edwin Aldrin walitumia chombo cha kusafiria katika anga za mbali kwa jina la Apolo- 11 na kufika mwezini na baadaye wakarejea duniani huku wakiwa na sampuli za mawe na udongo walizokuja nazo katika safari hiyo.

Kwa utaratibu huo juhudi kubwa za mwanadamu zilizokuwa zikifanywa kwa muda mrefu kwa lengo la kufikia mwezini zikawa zimezaa matunda.  ***

Na miaka 52 iliyopita katika siku kama ya leo, wanajeshi wa Uturuki walivamia na kukalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Cyprus, mashariki mwa kisiwa hicho.

Tangu kale Waturuki na Wagiriki wa Cyprus walikuwa wakizozana juu ya namna gani pande mbili hizo zigawane mamlaka ya nchi hiyo.