Mchambuzi wa Asia Magharibi: Israel inakabiliwa na changamoto chungu nzima
Mtaalamu wa masuala ya Asia Magharibi amesisitiza: “Tatizo kubwa zaidi la ndani linaloukabili utawala wa Kizayuni katika hali ya sasa ni matatizo ya kijamii ndani ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.
Hayo yameelezwa na Yunes Esmailzadeh na kusisitiza kwamba, matatizo ya kijamii, mgogoro wa migawanyiko, kudhoofika mfumo wa mahakama, uteuzi wa Netanyahu na kuchoka jeshi ni miongoni mwa changamoto kuu zinazoukabili utawala wa Kizayuni wa Israel hivi sasa.
Mtaalamu huyo wa masuala ya Asia Magharibi amebainisha kwamba, katika siku za hivi karibuni, maeneo yanayokaliwa kwa mabavu yameshuhudia kuongezeka tofauti na mvutano miongoni mwa vyama mbalimbali vya Kizayuni, huku vikielekea katika maandalizi ya uchaguzi wa bunge.
Katika hali hiyo, Benjamin Netanyahu, ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Likud, ameingia katika migogoro hata na baadhi ya washirika wake wa zamani, ambao sasa anawaona kuwa wapinzani wake wa kisiasa.
Ameongeza kuwa: “Serikali ya Trump, kwa kushirikiana na utawala wa Kizayuni na kwa kuungwa mkono na baadhi ya nchi za Kiarabu, iliishambulia Iran. Hata hivyo, tukirejea matukio yaliyotokea na mipango yao ya kimkakati, jambo walilolitarajia halikutokea.
Aidha amesema, Marekani na utawala wa Kizayuni zilikusudia kuishinda na kuidhoofisha Iran, kutekeza mpango wao wa kimkakati wa kuangamiza Muqawama na kuendeleza juhudi za kikanda za kupanua mchakato wa kuhalalisha uhusiano kati ya Israel na nchi jirani lakini zimeshindwa kufikia malengo yao na kuzidisha changamoto zaidi kwa Netanyahu na serikali yake inayolegalega.