Umoja wa Mataifa: Hakuna sehemu salama katika Ukanda wa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141256-umoja_wa_mataifa_hakuna_sehemu_salama_katika_ukanda_wa_gaza
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, hakuna sehemu salama katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.
(last modified 2026-09-07T02:59:20+00:00 )
Sep 07, 2026 02:56 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Hakuna sehemu salama katika Ukanda wa Gaza

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, hakuna sehemu salama katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Ripoti ya hivi karibuni ya Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu inasema kuwa, licha ya kupita karibu mwaka mmoja tangu kutangazwa makubaliano ya kusitisha mapigano, hakuna eneo wala mtu yeyote katika Ukanda wa Gaza aliye salama kutokana na mashambulizi yanayoendelea kuufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, ikieleza kuhusu kuongezeka mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza na kuuawa au kujeruhiwa watoto na wanawake kutokana na mashambulizi hayo, imetangaza kwamba hakuna eneo lolote salama katika Gaza, wala hakuna mtu aliye salama kutokana na mashambulizi ya Tel Aviv.

Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena umesema una wasi wasi mkubwa juu ya hali mbaya sana ya maisha katika Ukanda wa Ghaza sambamba na kushadidi mashambulizi ya mabomu na makombora yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina wa eneo hilo lililowekewa mzingiro.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na la Afya Duniani (WHO) yameonya kuhusu kuzorota hali ya kibinadamu katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kimabavu na Israel.

Ripoti zinaonyesha kuwa, theluthi mbili ya wakazi wa Gaza bado wanakabiliwa na viwango vya dharura vya njaa, na bila kuongezeka msaada wa kibinadamu, hadi asilimia 90 ya wakazi wanaweza kukabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu mkali wa chakula kabla ya mwisho wa mwaka huu.