Wanaharakati Kenya waituhumu serikali kwa kupuuza amri ya mahakama
-
Wanaharakati Kenya waituhumu serikali kwa kupuuza amri ya mahakama
Wanaharakati nchini Kenya wamezituhumu mamlaka za nchi hiyo kwa kukiuka amri ya mahakama iliyozuia kuanzishwa kituo cha karantini kwa wagonjwa wa Ebola
Matamshi hayo ni baada ya ripoti kusambaa kuwa raia kadhaa wa Marekani wamewekwa karantini katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Taasisi mbili za kiraia zilifungua kesi mahakamani mwezi uliopita kupinga kuanzishwa kituo hicho na mahakama iliamuru serikali kusitisha mipango yote iliyokuwepo.
Hata hivyo, wiki iliyopita, shirika moja la hisani la Marekani lilisema kwamba wafanyakazi wake 7 waliokuwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamewekwa karantini ya siku 21 nchini Kenya.
Vyombo vya habari vya Kenya vimeripoti kuwa, wafanyakazi hao waliwekwa kwenye kambi ya jeshi ya Laikipia, mahala ambako paliteuliwa hapo kabla kujengwa kituo cha karantini.
Mashirika yaliyofungua kesi ya kupinga kituo hicho ambayo ni Taasisi ya Katiba na Chama cha Wanasheria wa Kenya, yamekosoa vikali taarifa hizo yakisema zinaonesha kuwa, serikali imepuuza amri ya mahakama.
Hatua ya kuwaweka Wamarekani hao karantini nchini Kenya imezua utata mkubwa wa kisiasa na kisheria. Wanaharakati, wanasheria (LSK), na viongozi wa upinzani wamekosoa vikali hatua hiyo, wakidai serikali imepuuza amri halali ya mahakama na kuhatarisha afya ya umma. Hadi sasa, serikali ya Kenya haijatoa taarifa rasmi kuhusu utekelezaji wa mpango huo, licha ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuthibitisha uwepo wao humo.