Jumapili, 19 Julai, 2026
Leo ni Jumapili 4 Mfunguo Tano Safar 1448 Hijria mwafaka na 19 Julai 2026 Miladia.
Miaka 133 iliyopita alizaliwa malenga wa Russia kwa jina la Vladimir Mayakovsky. Mashairi ya Mayakovsky yalikuwa na nafasi kuu wakati wa mapinduzi ya Kikomonisti ya Urusi ya zamani mwaka 1917. Vladimir Mayakovsky alikuwa akiamini kuwa fasihi inapasa kuwa lugha ya watu wengi na inayobainisha maisha yao ya kijamii. ***
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, nchi ya Laos iliyopo katikati mwa Asia, ilipata uhuru kutoka kwa Ufaransa. Nchi ya Laos yenye milima mingi, ipo baina ya Vietnam, Cambodia, Thailand, Myanmar na China huku ikiwa na jamii ya watu milioni tano. Kwa miaka mingi, nchi hiyo ilikuwa ikitawaliwa na uongozi wa kifalme. Mji mkuu wa nchi hiyo Vientiane una ukubwa wa kilometa 237 huku ukiwa kando ya mto maarufu wa Mekong. Laos haipakani na bahari yoyote, na chanzo chake kikuu cha maji ni mto huo wa Mekong. ***
Katika siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, Kuwait ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Katika kipindi cha utawala wa Achaemenid, Kuwait ilikuwa ikihesabiwa kuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Mwaka 1899 Miladia, Kuwait iliwekeana saini na Uingereza, suala lililoifungulia London mlango wa kuikoloni nchi hiyo. Mwenendo huo uliendelea hadi baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Kuwepo kwa visima vya mafuta kulipanua uingiliaji mkubwa wa mashirika mengi ya Uingereza na Marekani katika taifa hilo. Hatimaye mwaka 1961 Kuwait na Uingereza zilitiliana saini makubaliano yaliyoifanya nchi hiyo kujipatia uhuru wake. ***
Miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo mapinduzi ya wananchi wa Nicaragua yalipata ushindi dhidi ya dikteta Anastasio Somoza wa nchi hiyo na muitifaki wake mkubwa yaani Marekani. Dikteta huyo kibaraka wa Marekani alichukua hatamu za uongozi wa Nicaragua mwaka 1967 na tangu wakati huo wimbi kubwa la upinzani lilianza kuenea nchini kote na katika America ya Kati dhidi ya kiongozi huyo. Mapambano ya silaha ya wapiganaji wa msituni ya Harakati ya Ukombozi wa Kitaifa ya Sandinista (FSLN) yaliyoanza mwaka 1963 yalipamba moto zaidi katikati ya muongo wa 1970 na kuungwa mkono na wananchi. Hatimaye Somoza alilazimika kukimbia nchi baada ya jeshi la Sandinista kuingia Managua mji mkuu wa Nicaragua katika siku kama ya leo. Karibu watu elfu 40 waliuawa katika mapinduzi ya Nicaragua. ***
Miaka 18 iliyopita katika siku kama ya leo, Khosro Shakibaei, mmoja wa waigizaji maarufu wa filamu na televisheni nchini Iran, alifariki dunia. Alizaliwa tarehe (7 Farvardin 1323 kwa kalenda ya Hijria Shamsia) katika Mtaa wa Molavi, mjini Tehran. Jina lake rasmi lililosajiliwa lilikuwa Khosro, lakini familia yake na watu wa karibu walimwita Mahmoud. Baba yake alikuwa afisa wa jeshi mwenye cheo cha Meja. Khosro alipokuwa na umri wa miaka 14, baba yake alifariki dunia kutokana na ugonjwa wa saratani. Akiwa na umri wa miaka 19, alipanda kwa mara ya kwanza jukwaani kuigiza katika tamthilia. Kutokana na kipaji chake na uigizaji uliovutia, baada ya muda mfupi akawa mwigizaji wa kitaalamu wa ukumbi wa michezo. Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, shughuli zake zilijikita katika uigizaji wa tamthilia pekee. Alianza kazi yake ya kitaalamu katika filamu mwaka 1982 kwa kuigiza katika filamu "Khat-e Qermez" (Mstari Mwekundu) iliyoongozwa na Masoud Kimiai. Katika maisha yake ya kisanii aliigiza katika karibu filamu 40 za sinema.