Mamilioni wamiminika mitaani Iran kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136504-mamilioni_wamiminika_mitaani_iran_kuadhimisha_ushindi_wa_mapinduzi_ya_kiislamu
Mamilioni ya wananchi kutoka matabaka yote ya kijamii wamejitokeza mitaani kote nchini Iran kushiriki maandamano ya kitaifa yanayoashiria maadhimisho ya miaka 47 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
(last modified 2026-02-11T07:08:25+00:00 )
Feb 11, 2026 07:08 UTC
  • Wananchi wa Iran wamejitokeza kwa mamilioni kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu
    Wananchi wa Iran wamejitokeza kwa mamilioni kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Mamilioni ya wananchi kutoka matabaka yote ya kijamii wamejitokeza mitaani kote nchini Iran kushiriki maandamano ya kitaifa yanayoashiria maadhimisho ya miaka 47 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa taarifa, umati wa watu ulianza kukusanyika mapema Jumatano asubuhi katika njia zilizopangwa jijini Tehran na katika zaidi ya miji na vitongoji elfu moja kote nchini. Washiriki walipangwa kuanza mkusanyiko wao kuanzia saa 3:30 asubuhi kwa saa za Iran, kisha kuelekea katika maeneo makuu ya mikusanyiko, yakiwemo Uwanja wa Azadi jijini Tehran, ambako Rais Masoud Pezeshkian anatarajiwa kutoa hotuba.

Waandaaji wa hafla hizo wamesema kuwa zaidi ya maeneo 1,400 kote nchini yanaandaa maandamano hayo ya mamilioni. Takwimu rasmi pia zinaonyesha kuwa takribani waandishi wa habari 7,200 wa ndani na karibu wawakilishi 200 wa vyombo vya habari vya kigeni wanaripoti matukio hayo ili kuonyesha kiwango cha ushiriki wa wananchi na shughuli zinazofanyika.

Usiku wa Jumanne, wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi waliinua sauti zao kwa kutamka “Allahu Akbar” saa 3:00 usiku, kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi. Katika miji mingi, hususan Tehran, mikusanyiko ya hiari ya wananchi waliobeba bendera za Iran ilishuhudiwa katika viwanja na maeneo ya umma.

Katika siku zilizotangulia maandamano haya, maafisa wa serikali na taasisi mbalimbali walitoa taarifa wakihimiza wananchi kushiriki kwa wingi. Mamlaka zimeeleza kuwa ushiriki huo ni ishara ya umoja wa kitaifa, subira na msimamo thabiti wa wananchi mbele ya mashinikizo ya nje. Wachambuzi wanaona kuwa maadhimisho haya pia hubeba ujumbe wa kisiasa na kitamaduni unaolenga kuonyesha mshikamano wa jamii na uwepo hai wa wananchi katika maisha ya taifa.

Ikumbukwe kuwa mnamo Januari 8 na 9, waibua ghasia wenye silaha walioungwa mkono na mataifa ya kigeni na makundi ya kigaidi waliteka nyara maandamano ya amani yaliyokuwa yameibuka kutokana na malalamiko ya kiuchumi, na kusababisha uharibifu mkubwa wa maduka, taasisi za serikali na huduma za umma, pamoja na kuuawa au kujeruhiwa kwa maelfu ya watu, wakiwemo raia na maafisa wa usalama.

Wananchi wa Iran katika matembezi ya kuadhmisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Mamlaka za Iran zimethibitisha kuwa mashirika ya kijasusi ya Marekani na Israel yalihusika moja kwa moja, yakitoa ufadhili, mafunzo na uungaji mkono wa vyombo vya habari kwa wahusika wa machafuko hayo. Kwa mujibu wa taarifa ya mwezi uliopita ya Taasis ya Mashahidi na Mavetarani Vita ya Iran, jumla ya watu 3,117 walipoteza maisha yao wakati wa ghasia hizo, wakiwemo raia wasio na hatia 2,427 pamoja na maafisa wa usalama.

Siku ya Jumatatu, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei aliwataka wananchi wa Iran kuonyesha azma, umoja na msimamo thabiti katika maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi, akisema kuwa mshikamano huo utawavunja moyo maadui wa taifa.

Familia katika matembezi ya maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Maandamano haya yanaadhimisha ushindi wa wananchi wa Iran dhidi ya udikteta wa Pahlavi, uliokuwa ukiungwa mkono kikamilifu na Marekani, katika majira ya baridi ya mwaka 1979. Imam Khomeini (MA) alirejea nchini kutoka uhamishoni tarehe 1 Februari 1979, akipokelewa kwa shangwe kubwa za wananchi, wiki chache baada ya shah kuondoka nchini katikati ya Januari.

Hatima ya utawala wa Pahlavi ilifungwa rasmi tarehe 11 Februari 1979, pale jeshi lilipoacha utii wake kwa shah na kujiunga na Mapinduzi ya Kiislamu.