Rais wa Colombia asema amenusurika jaribio la mauaji
https://parstoday.ir/sw/news/world-i136508-rais_wa_colombia_asema_amenusurika_jaribio_la_mauaji
Rais Gustavo Petro wa Colombia amesema alinusurika jaribio la mauaji jana Jumanne, baada ya miezi kadhaa ya maonyo kuhusu njama inayomlenga ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
(last modified 2026-02-11T09:32:07+00:00 )
Feb 11, 2026 09:32 UTC
  • Gustavo Petro
    Gustavo Petro

Rais Gustavo Petro wa Colombia amesema alinusurika jaribio la mauaji jana Jumanne, baada ya miezi kadhaa ya maonyo kuhusu njama inayomlenga ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

Gustavo Petro ameeleza kwamba helikopta yake haikuweza kutua Jumatatu usiku kuelekea pwani ya Karibea, kutokana na hofu kwamba watu - ambao hakuwataja majina - "wangeipiga risasi".

"Tulielekea kwenye ukanda wa bahari kwa saa nne na kuishia mahali ambapo hatukukusudia kwenda, tukikimbia kuuawa," amesema Rais Petro katika mkutano wa serikali uliorushwa hewani moja kwa moja.

Matamshi ya Rais Gustavo Petro wa Colombia yamekuja baada ya kutoweka kwa muda Seneta Aida Marina Quilcué, mwanamke wa kiasili na mshirika wa kisiasa wa Petro, na kumfanya rais kuzungumzia awamu mpya ya kutokuwa na uhakika wa kisiasa.

Matamshi ya Petro pia yanakuja huku kukiwa na ongezeko la vurugu nchini Colombia, miezi kadhaa kabla ya uchaguzi wa rais wa mwezi Mei, katika nchi ambayo imekuwa ikikumbwa na mizozo kwa miongo kadhaa kati ya waasi na makundi yenye silaha.

Petro, ambaye kikatiba hawezi kugombea muhula wa pili, amesema magenge ya biashara haramu ya dawa za kulevya yamekuwa yakijaribu kumuua tangu alipochukua madaraka mnamo Agosti 2022.

Viongozi wengi wa mrengo wa kushoto, wakiwemo wagombea urais, wameuawa nchini Colombia. Petro, rais wa kwanza wa mrengo wa kushoto nchini humo, alitangaza mwaka wa 2024 kwamba alinusurika jaribio la mauaji.