Kashfa ya Epstein ilivyofichua mmomonyoko wa kimaadili katika nchi za Magharibi
-
Kashfa ya Epstein ilivyofichua mmomonyoko wa kimaadili katika nchi za Magharibi
Wimbi la kujiuzulu linaloshuhudiwa huko Downing Street, kuanzia mkuu wa wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza hadi mkurugenzi wake wa mawasiliano, ni ishara za nje za mgogoro mkubwa wa kimaadili miongoni mwa wasomi na viongozi wa Magharibi.
Kesi ya Jeffrey Epstein, mlanguzi wa ngono na bilionea aliyehusishwa na mtandao wa wanasiasa, wanadiplomasia na matajiri, imezusha tetemeko la kisiasa barani Ulaya. Hata hivyo nchini Marekani, chanzo cha awali cha kashfa hiyo, kivitendo makali ya kadhia ya kashfa ya Epstein yamepunguzwa na kuwa jambo linaloweza kudhibitiwa. Tofauti hii, zaidi ya kitu kingine chochote, inafichua suara ya "ufisadi wa kimuundo" katika mfumo wa madaraka wa Magharibi.
Nchini Uingereza, mashinikizo ya maoni ya umma na utaratibu wa Bunge yamemfikisha Keir Starmer, ambaye aliingia madarakani akiwa na kaulimbiu ya kusafisha siasa, katika hatua ambapo uwaziri wake mkuu unaoendelea kukabiliwa na mashaka makubwa. Uchunguzi wa maoni uliofanywa na YouGov unaonyesha kwamba, karibu 50% ya wapiga kura wanataka Starmer ajiuzulu, huku 25% pekee wakiamini anastahili kuendelea kuwa waziri mkuu. Mgogoro kuhusu Balozi wa Uingereza huko Washington, Peter Mandelson, umeonyesha kwamba kile kilichoonekana hapo awali kama tatizo la kawaida la waziri mkuu sasa kimekuwa tishio kubwa kwa nafasi ya Starmer mwenyewe.
Kosa la Keir Starmer halikuwa katika kutenda uhalifu, bali katika kuanzisha uhusiano na mtu kama Peter Mandelson, mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa wa chama cha Labour ambaye kwa miaka mingi alificha au kufifiza umuhimu wa uhusiano wake na Epstein. Katika mfumo wa Westminster, "kufumbia macho huku kwa makusudi" kunatosha kudhoofisha uhalali wa kisiasa. Kufukuzwa kwa balozi Mandelson kunaweza kuonekana kama juhudi zilizofanyika kwa kuchelewa za kujaribu kulinda walau sura ya kidhahiri tu ya afya ya kimaadili katika siasa za Uingereza. Jitihada hizo ambazo, ingawa zina gharama kubwa, lakini bado zinaonyesha kwamba Ulaya inajali, walau kimaonyesho, ufisadi wa tabaka la watu mashuhuri.
Lakini upande wa pili wa Atlantiki, hali ni tofauti kabisa. Sio tu kwamba Marekani haijakumbana na mporomoko mkubwa ya kisiasa, lakini pia watu wengi waliotajwa katika nyaraka na faili la mlanguzi wa ngono, Jeffrey Epstein, wanaendelea kushikilia nyadhifa zao za kisiasa na ushawishi wa pesa. Huko Marekani ufuska na ufisadi havionekani kama ni kupotoka, bali ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa madaraka. Mfumo wa kisiasa wa Marekani umeunganishwa sana na ushawishi wa kifedha, mitandao ya usalama na maslahi ya vyama kiasi kwamba kashfa za kimaadili, hata katika kiwango chake cha juu zaidi kama zile za Epstein, haziwezi kumuwajibisha mhusika. Hapa ndipo dhana ya "kuwakingia kifua watu mashuhuri" inapobadilika kutoka madai matupu na kuwa hali halisi.
Faili la Epstein limeonyesha jinsi baadhi ya watu mashuhuri na wenye madaraka huko Magharibi wanavyohusika katika unyanyasaji uliopangwa, ndani ya muktadha wa muundo wa madaraka. Hii si hadithi ya mhalifu mmoja wa ulanguzi wa ngono tu. Ni simulizi ya mtandao unaohusisha siasa, uchumi, vyombo vya habari na hata taasisi za mahakama. Majina ya wahusika katika uhalifu na kashfa hiyo yanapochujwa na kufichwa, uchunguzi ukasitishwa, na maoni ya umma yanapopindishwa na kuelekezwa kwenye migogoro ya kubuni au ya kiusalama, jambo hilo haliwezi tena kuwa kadhia ya kutokea kwa sadfa na mara moja tu; Huu ni mpangilio wa kimfumo.
Katika muktadha huu, matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov, ingawa yaliambatana na lugha kali na malengo mahususi, lakini yanagusa jeraha halisi. Sergei Lavrov amekutaja kufichuliwa nyaraka za Epstein kuwa si kashfa ya kimaadili tu, bali ishara ya "ufisadi wa kimuundo wa watu mashuhuri wa Magharibi," na kusema, kunafichua sura halisi ya Magharibi. Msimamo huu unaashiria ukweli kwamba, kesi ya Epstein ni kielelezo cha kudhoofika uhalali wa kimaadili wa Magharibi katika ngazi ya kimataifa. Naam, Magharibi, ambayo inajinadi kama mtetezi wa haki za binadamu, hukaa kimya bali huficha uhalifu unaofanywa na wasomi, viongozi na wanasiasa wake au kuufifiza na kuudogesha.
Jambo muhimu na la kupewa mazingatio hapa ni kwamba, hata msimamo mkali wa Ulaya katika kadhia hii hauna maana ya kuwa salama kimaadili. Kwani, kujiuzulu wanasiasa wanaohusishwa na faili la ulanguzi wa ngono wa watoto wadogo na kuomba msamaha, kama hakutasababisha mageuzi ya miundo ya madaraka, kutakuwa sawa na kidonge cha kutuliza maumivu badala ya kuponya ugonjwa.
Kashfa ya Epstein imeonyesha jinsi watu mashuhuri na wenye madaraka na pesa huko Magharibi wanavyofunikana na kukingiana kifua katika mtandao uliofungwa, kuanzia taarifa nyeti hadi mahusiano ya kibinafsi. Tofauti kati ya Ulaya na Marekani zaidi iko katika "usimamizi wa kashfa" kuliko katika asili yake. Ulaya bado inapaswa kulipa gharama za kisiasa za kakshfa kama hizo, lakini Marekani imeweza kupunguza gharama hizo.
Mwishoni, tunasema kuwa faili la Jeffrey Epstein ni kioo kinachofichua pengo kati ya kuwa na madai ya maadili na uhalisia wa ukatili wa madaraka.