Iran: US inatumia vikwazo kuwanyamazisha wanaokosoa mauaji ya halaiki Gaza
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Esmaeil Baghaei amesema Marekani inajaribu kuwanyamazisha wakosoaji wa mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Gaza kwa kuwawekea vikwazo.
Baghaei amesema hayo akijibu taarifa iliyotolewa jana Jumatano na Josep Borrell, mkuu wa zamani wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X.
"Na hii ni sambamba na vikwazo vya Marekani dhidi ya Ripota Maalum wa Palestina, Francesca Albanese, ili kuwanyamazisha wakosoaji wowote wa mauaji ya kimbari na ukatili wa Israel huko Gaza na Ukingo wa Magharibi," ameandika Baghaei.
"Ukweli hauwezi kukandamizwa na vikwazo,” Baghaei amesema katika ujumbe huo alioutuma kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X na kuongeza kuwa, "Francesca Albanese anaonewa na kuwekewa vikwazo kwa kusema ukweli na kusimama dhidi ya mauaji ya kimbari, uvamizi na ubaguzi wa rangi."
Mapema jana, Borrell alitoa wito kwa Umoja wa Ulaya kumuunga mkono Albanese baada ya Marekani kumlenga kwa vikwazo kinyume cha sheria afisa huyo wa Umoja wa Mataifa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Borrell alisema hatua hiyo ghalati ya Washington dhidi ya Albanese ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, EU inafungwa na mikataba yake inayoitaka iheshimu sheria za kimataifa na kuwalinda wote walio na mamlaka ya Umoja wa Mataifa.
Albanese amekuwa mkosoaji mkubwa wa ukatili wa Israel huko Gaza, ambapo zaidi ya Wapalestina 58,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa shahidi katika mashambulizi ya Israel tangu Oktoba 7, 2023.