Wakati Trump Anapokiuka Hata Ahadi Alizotoa kwa Washirika wake wa Kikanda!
Rais Donald Trump wa Marekani amekiuka ahadi yake ya awali kwa Saudi Arabia kwa kutangaza masharti mapya ya utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia kati ya nchi hizo mbili.
Masaa 24 tu baada ya kusainiwa makubaliano ya ushirikiano wa nyuklia kwa matumizi ya kiraia kati ya Marekani na Saudi Arabia, Trump alitangaza muda mfupi baadaye kuwa makubaliano hayo yataendelea tu iwapo Riyadh itajiunga na Mapatano ya Abraham (Abraham Accord). Hatua hii imewashangaza sana watawala wa Saudia, ambao hawakutarajia hali hii ijitokeze. Trump ametangaza hadharani kwamba kuanzishwa mahusiano ya kawaida na utawala ghasibu wa Israel ni sharti la kuendelezwa makubaliano hayo ya kuiruhusu Saudi Arabia irutubishe urani.
Trump anasisitiza kwamba makubaliano ambayo yanakamilika kwa sasa kati ya Idara ya Nishati ya Marekani na Saudi Arabia yanahusu tu matumizi ya kiraia ya nishati ya nyuklia na wala hayajumuishi urutubishaji wa urani.
Katika ujumbe huo, ambao unaweza kuchukuliwa kama kukiri kimyakimya kuhusu malengo ya kiraia ya mpango wa nyuklia wa Iran, ameandika: "Makubaliano ya mipango ya kiraia ya nyuklia ambayo kwa sasa yanajadiliwa kati ya Idara ya Nishati ya Marekani na Saudi Arabia, na itatumika tu kwa malengo ya kiraia, sawa na mipango ambayo inatekelezwa kwa sasa na Iran, UAE, na wengine ambao tayari wanaimiliki, yataidhinishwa." Trump amedai kuwa Marekani haina pingamizi yoyote na vituo vya nyuklia vya kiraia ambavyo havihusishi urutubishaji.
Hatimaye alifichua dhamira yake halisi, aliposema: "Lakini hili linategemea kikamilifu iwapo Saudi Arabia itajiunga na 'Makubaliano ya Abraham' ambayo yanaheshimika na yamekuwa na mafanikio makubwa."
Trump amekiri asili ya kiraia ya mpango wa nyuklia wa Iran, ingawa amekuwa akiashiria mara kwa mara madai ya kuizuia Iran kupata silaha za nyuklia kama kisingizio cha kuhalalisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya nchi hii. Kuhusu makubaliano ya nishati ya nyuklia na Saudi Arabia, ambayo yamefikiwa baada ya juhudi za miongo miwili na yaliyolenga kuyapa mashirika ya Marekani fursa kubwa ya kushiriki katika mpango wa nishati ya nyuklia wa Riyadh, Trump, kama kawaida yake amejiondoa ghafla katika makubaliano hayo. Bila kutoa taarifa yoyote, ameweka sharti jipya la ghafla ambalo alijua fika kwamba halitakubaliwa na Saudia, ikitiliwa maanani msimamo wa muda mrefu wa Riyadh wa kutoutambua rasmi utawala wa Israel hadi pale taifa huru la Palestina litakapoundwa. Kwa maneno mengine, Trump alitia saini makubaliano ambayo alijua vizuri kuwa hayangetekelezeka, isipokuwa kama Saudi Arabia ingeamua kuachana na msimamo wake wa awali. Hii ndiyo maana halisi ya kuvunja ahadi na kumsaliti mshirika. Mbinu ya Trump kuhusu Saudi Arabia inafuata mtindo unaojulikana vizuri. Katika muhula wake wa kwanza, alijiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na Iran, ingawa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ulikuwa umethibitisha mara kwa mara kwamba Iran inafuatilia mpango wake wa nyuklia kwa malengo ya amani. Aliweka ushuru mkubwa kwa bidhaa za washirika wake wa Ulaya na kujiondoa katika mikataba mingi muhimu ya kimataifa. Kuhusu washirika wa Washington Asia Magharibi, pia, sera zake zimekuwa zikijikita zaidi katika kutumia mashinikizo na ulaghai badala ya uaminifu au ushirikiano wa kudumu.
Wachambuzi wanaamini kwamba Trump amepuuzilia mbali makubaliano ya nyuklia na Saudi Arabia kufuatia wimbi la ukosoaji kutoka kwa wataalamu wa kihafidhina na vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na Fox News na The Wall Street Journal. Badala ya kukabiliana na wakosoaji wake wa ndani, amehamishia gharama ya hatua hiyo ya kulegeza msimamo kwa mshirika wake wa kimkakati. Iliripotiwa kwamba Waziri wa Nishati wa Marekani alitangaza makubaliano hayo bila Trump kujua, na hasira ya Rais ikachochewa na uamuzi huo wa haraka. Tabia kama hiyo inaonyesha kuwa Trump hutanguliza maslahi yake binafsi na ya kisiasa mbele ya ahadi za kimataifa.
Hatua ya Trump kuhusiana na Saudi Arabia inatoa ujumbe wa wazi kwa washirika wote wa Marekani katika eneo kwamba hakuna makubaliano yoyote naye yanaweza kuaminika. Ikiwa anaweza kukanusha na kubatilisha saa chache tu baadaye makubaliano yaliyotiwa saini na waziri wake, ni vipi ahadi zake nyingine zinaweza kuaminika? Gazeti la Washington Post limeripoti kuwa hata washirika wake wa Ghuba ya Uajemi wanajitenga taratibu na Washington, hali inayochochewa pakubwa na tabia isiyotabirika wala kuaminika ya Trump.
Suala la makubaliano ya nyuklia na Saudi Arabia ni mfano mwingine wa rais anayekiukakiuka ahadi zake na kukosa sifa ya uaminifu. Trump ameonyesha kivitendo kuwa haheshimu ahadi yoyote, hata na washirika wake wa kimkakati na kwamba yuko tayari kuvunja ahadi yoyote iwapo itagongana na maslahi ya muda mfupi au kukabiliwa na mashinikizo ya vyombo vya habari. Tabia hii haiharibu tu itibari ya Marekani katika eneo, bali pia unaibua shaka kubwa kuhusu uhalali na ukweli wa ahadi za Washington katika eneo. Saudi Arabia na washirika wengine wa kieneo wa Marekani sasa wamejifunza kikamilifu somo kwamba ahadi za Trump hazina thamani zaidi ya kuwa ni machapisho tu ya muda mfupi na yenye utata katika mitandao ya kijamii, hasa kwenye mtandao wa Truth Social.