ICC yapuuza mashinikizo ya US, Israel; haitatengua waranti dhidi ya Netanyahu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128418
Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) wameamua kwamba hati zilizotolewa na korti hiyo ya mjini The Hague za kukamatwa Waziri Mkuu wa utawala wa Israel na waziri wake wa zamani wa vita zingalipo, huku wakikaidi mashinikizo makubwa ya Israel na Marekani ya kufutulia mbali waranti hizo.
(last modified 2025-07-21T07:45:22+00:00 )
Jul 17, 2025 04:21 UTC
  • ICC yapuuza mashinikizo ya US, Israel; haitatengua waranti dhidi ya Netanyahu

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) wameamua kwamba hati zilizotolewa na korti hiyo ya mjini The Hague za kukamatwa Waziri Mkuu wa utawala wa Israel na waziri wake wa zamani wa vita zingalipo, huku wakikaidi mashinikizo makubwa ya Israel na Marekani ya kufutulia mbali waranti hizo.

Majaji hao walitupilia mbali maombi hayo jana Jumatano kuhusiana na vibali vilivyotolewa Novemba mwaka jana vya kukamatwa Benjamin Netanyahu na Yoav Gallant kwa uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu, na kutumia njaa kama silaha dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Maagizo hayo yalitolewa Novemba 21 kutokana na hatua za wawili hao aidha kusababisha, kurefusha au kushajiisha vita vya mauaji ya halaiki vilivyoanza Octoba 2023 huko Gaza, ambavyo hadi sasa vimeua zaidi ya Wapalestina 58,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Majaji hao wa ICC wamesema hati hizo zina itibari na zitaendelea kutumika, huku mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa ikiendelea kukagua kile kinachoitwa mapingamizi ya utawala wa Kizayuni kwa mamlaka ya ICC katika kesi hiyo.

Mbali na Marekani na Israel, lakini uamuzi wa mahakama hiyo wa kutoa waranti dhidi ya Netanyahu na Gallant umezitia nchi nyingi za Ulaya, ambazo karibu zote ni wanachama wa mahakama hiyo, katika hali ngumu. Nchi hizo sasa zinakabiliwa na mtihani mkubwa.

Hata hivyo, misimamo ya nchi za Ulaya kuhusu kadhia hiyo ni ishara nyingine ya wazi kuhusu siasa zao za undumakuwili kuhusiana na masuala mbalimbali ya kimataifa.

Kadhalika majaji hao wa ICC wamepinga ombi la Israel la kusimamisha uchunguzi zaidi wa uhalifu unaofanywa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, na kusisitiza kukataa kwa mahakama hiyo kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya kidiplomasia.