Rais wa Nigeria athibitisha kuuawa afisa wa ngazi ya juu wa jeshi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133364-rais_wa_nigeria_athibitisha_kuuawa_afisa_wa_ngazi_ya_juu_wa_jeshi
Rais wa Nigeria amethibitisha kuwa Brigedia jenerali Musa Uba ameuawa na kundi la kigaidi akiwa matekani. Mauaji hayo yamefanywa siku chache baada ya afisa huyo wa ngazi ya juu wa jeshi la Nigeria kutekwa nyara na wanamgambo wa kundi la ISWAP kufuatia shambulio la kuvizia kaskazini mashariki mwa Jimbo la Borno ambalo pia liliwaua wanajeshi wanne.
(last modified 2025-11-19T12:24:00+00:00 )
Nov 19, 2025 12:24 UTC
  • Rais Bola Tinubu wa Nigeria
    Rais Bola Tinubu wa Nigeria

Rais wa Nigeria amethibitisha kuwa Brigedia jenerali Musa Uba ameuawa na kundi la kigaidi akiwa matekani. Mauaji hayo yamefanywa siku chache baada ya afisa huyo wa ngazi ya juu wa jeshi la Nigeria kutekwa nyara na wanamgambo wa kundi la ISWAP kufuatia shambulio la kuvizia kaskazini mashariki mwa Jimbo la Borno ambalo pia liliwaua wanajeshi wanne.

Rais Bola Tinubu wa Nigeria amethibitisha kifo cha Brigedia Jenerali Musa Uba katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bayo Onanuga. 

Rais wa Nigeria ametuma salamu za rambirambi na kutoa pole kwa jeshi na familia za wanajeshi wengine waliovamiwa na kuuawa Ijumaa iliyopita.

Awali vyanzo vya habari vya Nigeria viliarifu kuwa, Brigedia Jenerali Uba alitekwa nyara akiwa pamoja na wanajeshi wanne baada ya tawi la kundi la Boko Haram kwa jina la ISWAP kuushambulia msafara wake Ijumaa usiku, kaskazini mwa Chad. 

Awali jeshi la Nigeria lilikanusha kutekwa nyara afisa wake huyo na kudai kuwa alikuwa salama salimini baada ya wanajeshi kujibu hujuma ya magaidi. 

Kundi la ISWAP kwa upande wake Jumatatu lilitangaza kuwa limemteka nyara na kisha kumuuwa. Kundi hilo pia lilirusha picha mitandaoni ili kuthibitisha jinai hiyo. 

Rais wa Nigeria amesema amesikitishwa na kuhuzumishwa na vifo vya wanajeshi na maafisa hao waliokuwa katika majukumu yao ya kazi. 

Jeshi la Nigeria limekumbwa na changamoto katika mapambano yake dhidi ya ugaidi, lakini hii ni mara ya kwanza afisa wa jeshi wa cheo cha juu kukamatwa, kuhojiwa, na kisha kuuawa.