Nchi za Maziwa Makuu zaitangaza RSF kuwa ni kundi la kigaidi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imetangaza kwamba Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu uliofanyika Kinshasa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umeidhinisha pendekezo la kuvitangaza Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF kuwa ni "kundi la kigaidi."
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mkutano wa 9 wa Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu huko Kinshasa, umemaliza kazi yake kwa kutoa taarifa ya mwisho. Taarifa hiyo imejumuisha pendekezo la wazi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kulitaka lilaani jinai za Vikosi vya Msaada wa Haraka vya Sudan RSF.
Ujumbe wa Sudan umeongozwa na Ibrahim Jaber Ibrahim, mjumbe wa Baraza la Mpito la Utawala ambaye pia ni Naibu Amirijeshi Mkuu wa Jeshi la Sudan SAF. Maafisa kadhaa wa serikali na makamanda wa jeshi na masuala ya usalama wa Sudan nao wameshiriki kwenye mkutano huo wa Kinshasa.
Taarifa ya mwisho ya mkutano huo wa wakuu wa nchi za Maziwa Makuu ya Afrika imejikita zaidi kwenye masuala ya usalama na ulinzi ndani ya nchi wanachama, masuala yanayohusiana na wanawake na watoto pamoja na maendeleo ya kijamii na ulinzi wa rasilimali za madini za nchi wanachama kutokana na matumizi mabaya ya madini hayo ambayo yanaishia kwenye kufadhili jinai za vikundi vya waasi na wanamgambo wenye silaha katika eneo hilo.
Muawiya Othman Khalid, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan amesema kwamba, "mkutano huo umeidhinisha mapendekezo yaliyotolewa na Baraza la Mawaziri na Mawaziri wa Ulinzi na Usalama wa Sudan, ambao wote walisisitizia wajibu wa kutangazwa rasmi kwamba Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF ni kundi la kigaidi."