Jeshi la Sudan laondoka "Umm Sayala" huku mapigano makali yakiendelea Kordofan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133320-jeshi_la_sudan_laondoka_umm_sayala_huku_mapigano_makali_yakiendelea_kordofan
Chanzo cha kijeshi kimethibitisha kwamba jeshi la Sudan na vikosi washirika jana Jumatatu viliondoka katika mji wa Umm Sayala huko Darfur Kaskazini, saa chache baada ya kuukomboa kutoka kwa wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), huku mapigano yakiiendelea katika maeneo kadhaa ya eneo hilo.
(last modified 2025-11-18T07:06:19+00:00 )
Nov 18, 2025 07:06 UTC
  • Jeshi la Sudan
    Jeshi la Sudan

Chanzo cha kijeshi kimethibitisha kwamba jeshi la Sudan na vikosi washirika jana Jumatatu viliondoka katika mji wa Umm Sayala huko Darfur Kaskazini, saa chache baada ya kuukomboa kutoka kwa wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), huku mapigano yakiiendelea katika maeneo kadhaa ya eneo hilo.

Chanzo cha Vikosi vya Ngao ya Sudan, vinavyoshirikiana na jeshi, kimesema kwamba vikosi vyao vimeondoka Umm Sayala "kama hatua ya kimkakati."

Vyanzo hivyo vimeongeza kuwa kamanda wa Kikosi cha Ngao ya Sudan amejeruhiwa kidogo wakati wa mapigano katika eneo la Umm Sayala.

Kwa upande wake, Vikosi vya Msaada wa Haraka vimetangaza kwamba vimeudhibiti mji wa Umm Sayala huko Darfur Kaskazini baada ya "vita vikali" na kwamba jeshi la Sudan na washirika wake limepata hasara kubwa na hali na vifaa.

Awali jeshi la Sudan lilikuwa limethibitisha kwamba limeudhibiti tena mji huo baada ya mapigano na Vikosi vya Msaada wa Haraka.

Baada ya kudhibiti mji wa El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vimetuma sehemu kubwa ya wapiganaji wake katika jaribio la kudhibiti miji mikubwa katika eneo la Kordofan.
Chanzo cha kijeshi katika jeshi la Sudan kimesema kwamba vikosi vya jeshi vinapambana na waasi wa RSF katika miji kadhaa katika jimbo la Kordofan Kaskazini.

Tangu katikati ya Aprili 2023, Sudan imekuwa katika mzozo wa kijeshi kati ya jeshi la taifa na waasi wa RSF ambao umesababisha vifo vya makumi ya maelfu na watu na kuwalazimisha wengine milioni 13 kuhama makazi yao.