Mchambuzi: Utawala wa sasa wa Syria utaifanya nchi igawanyike vipande vipande
Mtafiti wa mahusiano ya kimataifa Yasser Al-Khatib amesema, hali ya mambo nchini Syria ni ngumu na tata mno kutokana na udhaifu wa watawala wake wa sasa, ambao unawasukuma watawala hao kutafuta msaada kutoka nje ya nchi, huku Wasyria wakighariki kwenye dimbwi la mgawanyiko wa nchi unaosababishwa na maslahi yanayokinzana ya nchi zinazoingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.
Al-Khatib, ameyasema hayo katika mahojiano na televisheni ya Al-Alam na kubainisha kwamba, matukio yanayojiri nchini Syria tangu baada ya Al-Jolani kurudi kutoka safari yake ya hivi karibuni huko Washington yamethibitisha kuwa, serikali mpya haijafikia maridhiano na wananchi wa Syria na haijafanya nao mazungumzo ya ndani ya kitaifa.
Mchambuzi huyo wa mahusiano ya kimataifa amefafanua kuwa, watu wote wenye uchungu na Syria wameshaitaka serikali mara kadhaa ifanye mazungumzo ya ndani, ya mpito wa kisiasa, kitaifa na kidemokrasia kwa sababu nchi hii inakabiliwa na migogoro mingi ambayo inahitaji kutatuliwa, lakini serikali hii, ambayo wajumbe wake hawajatokana na nchi hii, imepinga maombi hayo na kusababisha mgawanyiko miongoni mwa makabila na matabaka tofauti ya watu, na kuupa nguvu zaidi uwezekano wa nchi kugawanyika.
Al-Khatib ameendelea kueleza: "safari za al-Jolani katika nchi tofauti za dunia zinahusisha utoaji fursa na upendeleo wa kisiasa tu kwa nchi hizo ambao ni kwa madhara ya watu wa Syria, kwa hivyo tunashuhudia kusini mwa Syria ikitoka kwenye udhibiti wa serikali hii na badala yake kama waliokata kamba, Waisraeli ndio wanaojifaragua huko, wakiweka vituo vya upekuzi na vizuizi vya barabarani, na kuiendesha kusini mwa Syria vile ambavyo wao wanaona inafaa."
Ameongezea kwa kusema: "huko Damascus, kama tulivyoona jana, imetokea miripuko na majaribio ya kuwaua baadhi ya shakhsia, na makombora yamevurumishwa kutoka maeneo tofauti. Hata katika maeneo ya Al-Sahel, wataalamu wa kisayansi wanauawa kwa sababu za matapo na kwa utambulisho wao wa kidini; na leo gari moja lililengwa na shambulio la ndege isiyo na rubani. Masuala haya yote yanaonyesha kuwa Syria haina serikali kuu iliyo imara na mamlaka ya kujitawala, na yeyote aingiaye kutoka nje anaweza kufanya chochote huko atakacho.../