Maandamano dhidi ya al Jolani yaanza Syria
(last modified Sun, 22 Dec 2024 07:54:18 GMT )
Dec 22, 2024 07:54 UTC
  • Maandamano dhidi ya al Jolani yaanza Syria

Duru za habari zimeripoti kuwa kutekwa nyara raia wa Syria katika mkoa wa Halab nchini humo kumezushha cheche za awali za maandamano na malalamiko dhidi ya Muhammad al Jolani kamanda wa kundi la upinzani lenye silaha la Hay'at Tahrir al Sham(HTS).

Vyombo vya habari vyenye mfungamano na wapinzani wa Syria vimetangaza kuwa wakazi wengi wa mji wa Halab walikusanyika katika maidani ya Saadullah al Jabari wakilalamikia kutekwa nyara raia wa nchi hiyo na kundi la kigaidi la Tahrir al Sham.  

Baada ya maandamano hayo, vikosi vya Tahrir al-Sham viliwateka nyara  wanawake kadhaa ambao walitaka waume na ndugu zao waachiliwe huru kutoka katika jela za al Jolani. Familia za wanawake waliotekwa nyara katika mkoa wa Halab pia wameshika silaha na kuingia mitaani wakitaka kuachiwa huru wanawake hao.  

Waandamanaji wanaopinga vitendo vya kundi la Tahrir al-Sham huko Halab, Syria walimpa Jolani saa chache kuwaachilia huru wanawake waliotekwa nyara na wanamgambo wa kundi hilo. 

Wakati huo huo baadhi ya vyombo vya habari pia vimeripoti kuhusu kuzuka mapigano kati ya raia wa Syria na wanamgambo wa kundi la Tahrir al Sham. Watawala wapya wa Damascus hivi karibuni walimteua Abul Az Saraqeb kuwa Gavana wa mji wa Halab.