Gharibabadi: Nchi 3 za Ulaya zimejiondoa zenyewe kwenye diplomasia na Iran
Naibu Waziri wa Masuala ya Sheria na Masuala ya Kimataifa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran leo amesema wakati akijibu swali kutoka kwa mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la Fars kwamba, Iran itaendelea kuonesha ushirikiano na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kwa mujibu wa hatua zinazochukuliwa na Bodi ya Magavana ya wakala huo na kamwe haitofumbia macho haki yake ya kiimsingi ya kunufaika na teknolojia ya kisasa ya nyuklia.
Kazen Gharibabadi amesema kuhusu azimio lililopendekezwa na nchi tatu za Ulaya na Marekani kwenye mkutano wa wiki hii wa Bodi ya Magavana ya IAEA kwamba nchi hizo tatu za Ulaya zilijiondoa zenyewe kwenye mazungumzo na diplomasia na Iran kwa hatua ziliyochukua New York na kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kile kilichoitwa snapback. Amesema, tab'an nchi hizo tatu hazikufanikiwa kwenye njama yao hiyo ya snapback kwani jamii nzima ya kimataifa haikuunga mkono hatua yao. Ameongeza kuwa: Hivi sasa nchi hizo zinataka kuutumia mji wa Vienna kufidia kushindwa kwao huko New York.
Amesema cha kusikitisha ni kwamba vituo vya nyuklia vya Iran vilishambuliwa na Marekani huku nchi hizo hizo za Ulaya zikibaki kimya na wakati mwingine zikiunga mkono mashambulizi hayo. Cha kushangaza zaidi ni kwamba hata Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA nao umeshindwa angalau kulaani tu mashambulizi hayo ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran ambavyo vilikuwa chini ya uangamlizi wa IAEA.
Aidha amesema: Bila ya shaka, sababu ya njama hizi mpya za madola ya Magharibi ni kwamba mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran hayakuwa na athari ziliyotarajia kwa Iran na kwa jamii ya Iran. Athari zake ni chache sana tofauti na yalivyotarajia madola hayo ya kibeberu na ndio maana hivi sasa yanatumia Bodi ya Magavana ya IAEA kuishinikiza tena Iran kwa njia nyingine.