Kutopendelea IAEA upande wowote; takwa kuu la Iran katika kadhia ya nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i133248-kutopendelea_iaea_upande_wowote_takwa_kuu_la_iran_katika_kadhia_ya_nyuklia
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuhusu ripoti ya Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA: "lazima ripoti kama hizo zibaki daima kuwa za kitaalamu, zinazotokana na ukweli halisi, na zisizoathiriwa na utashi wowote wa kisiasa".
(last modified 2025-11-16T06:54:13+00:00 )
Nov 16, 2025 06:54 UTC
  • Kutopendelea IAEA upande wowote; takwa kuu la Iran katika kadhia ya nyuklia

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuhusu ripoti ya Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA: "lazima ripoti kama hizo zibaki daima kuwa za kitaalamu, zinazotokana na ukweli halisi, na zisizoathiriwa na utashi wowote wa kisiasa".

Amir Saeed Iravani, ameeleza hayo katika mkutano wa Baraza Kuu uliojadili ripoti ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na akaongezea kwa kusema: "wakati baadhi ya nchi zinazikwamisha kimfumo nchi zinazoendelea zisiweze kunufaika na teknolojia ya nyuklia inayotumiwa kwa malengo ya amani, wakati huohuo, nchi hizo zinaupatia silaha na misaada ya kijeshi utawala wa kizayuni, ambao si mwanachama wa Mkataba Unaopiga Marufuku Uenezaji Silaha za Nyuklia na una maghala ya siri ya silaha za mauaji ya halaiki".

Iravani amebainisha kuwa, kuzipatia nchi wanachama utaalamu na teknolojia ya nyuklia, ambako kumedhaminiwa na Kifungu cha 4 cha Mkataba Unaopiga Marufuku Uenezaji Silaha za Nyuklia na Hati ya IAEA, si kuzifanyia ihsani nchi hizo bali ni haki yao ya msingi na isiyoweza kufutwa.

Amir Saeid Iravani, Balozi wa Iran UN

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameendelea kueleza kwamba: mnamo mwezi Juni 2025, dunia ilishuhudia kitendo cha jinai na uchokozi mkubwa. Saa chache tu baada ya kupitishwa azimio lililochochewa na utashi wa kisiasa katika Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, utawala wa Kizayuni ulianzisha mashambulizi makubwa na makali dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran vilivyo chini ya ukaguzi na usimamizi kamili wa wakala huo. Mashambulizi hayo ya kijinai yaliwalenga wanasayansi wa Iran na familia zao, yakawaua na kuwajeruhi maelfu ya watu, na kusababisha hasara na uharibifu mkubwa wa vitu.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Iravani alisema: “Marekani, ambayo ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama na mtiaji saini wa NPT, ilijiunga na uchokozi huo wa Juni 22 na kuvilenga moja kwa moja vituo vilivyo chini ya usimamizi wa wakala wa IAEA. Vitendo hivyo vilikuwa ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, Mkataba wa Umoja wa Mataifa, Hati ya IAEA, na Azimio 487 la Baraza la Usalama la mwaka 1981; ambalo linakataza kwa uwazi kabisa kufanya shambulio la aina yoyote dhidi ya vituo vya nyuklia vilivyo chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kila mara kwamba Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki huwa unatoa ripoti zake kwa utashi na upendeleo, kwa sababu Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zinaitumia taasisi hiyo kwa malengo yao ya kisiasa dhidi ya nchi zenye misimamo huru; na badala ya kujikita kwenye masuala ya kiufundi, nchi hizo huzitumia ripoti hizo kama wenzo wa kuishinikiza Iran kidiplomasia na kuiwekea vikwazo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshatoa indhari mara kadhaa kwamba, Marekani na Troika ya Ulaya zimeutoa nje ya mkondo wa kiufundi mchakato wa kuchunguza faili lake la nyuklia na kuliingiza kwenye uga wa kisiasa kwa kuwasilisha maazimio dhidi ya Iran mbele ya Bodi ya Magavana ya IAEA. Baada ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, ripoti za wakala huo wa nishati ya atomiki, zimekuwa zikitumiwa kama kisingizio cha kushadidisha mashinikizo ya kiuchumi na kisiasa dhidi ya Iran.

Viongozi wa Iran wanasema, katika ripoti zake, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki umekuwa ukipuuza au kutoupa umuhimu unaostahiki ushirikiano mkubwa inaotoa Iran, ilhali Jamhuri ya Kiislamu imeshatangaza na kusisitiza mara kadhaa kwamba, shughuli zake za nyuklia zinafanyika kwa malengo ya amani na ziko chini ya usimamizi na ukaguzi wa wakala huo. Iran inatilia mkazo ulazima wa ripoti za IAEA kutoegemea upande wowote kwa sababu itibari ya taasisi hiyo itadumu endapo tu ripoti hizo zitakuwa za kitaalamu, zinazozingatia ukweli halisi, na kutochangaywa na mashinikizo kisiasa.

Kushoto: Mkuu wa AEOI, Mohammad Eslami na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi 

Troika ya Ulaya inayojumuisha Ufaransa, Ujerumani na Uingereza imeandaa rasimu ya azimio dhidi ya Iran itakayowasilishwa katika mkutano wa Bodi ya Magavana ya IAEA utakaofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 21 Novemba. Hatua za Marekani na Troika ya Ulaya dhidi ya Iran zinachukuliwa wakati Iran ingali inaendeleza maelewano ya kidiplomasia na kuendelea kutoa ushirikiane kwa IAEA, na kusisitiza kwamba iko tayari kufufua makubaliano ya JCPOA ikiwa pande zingine katika makubaliano hayo zitarejea kwenye utekelezaji wa ahadi na majukumu yao.

Makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni mjini Cairo kati ya Iran na IAEA ya kuanzisha tena ukaguzi wa kiufundi na mazungumzo ya kidiplomasia yaliyofanyika huko Geneva, Muscat na Roma yote hayo yanaonyesha nia njema ya Tehran ya kutatua suala hilo kwa njia za diplomasia, lakini kwa sharti la kuwepo hakikisho la kweli la kuondolewa vikwazo. Iran imeshasisitiza mara kadhaa kwamba, iko tayari kufikia makubaliano endelevu na ya kuaminika, lakini yatakayotoa dhamana na hakikisho la kuondolewa vikwazo ilivyowekewa na kuzuia kuja kutumiwa vibaya hakikisho hilo katika siku za baadaye.../