Bin Salman: Tunajaribu kupatanisha baina ya Iran na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i133350-bin_salman_tunajaribu_kupatanisha_baina_ya_iran_na_marekani
Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia ambaye kimsingi ndiye kiongozi nambari moja wa nchi hiyo amesema: "Tutafanya kila tunavyoweza kuhakikisha kunafikiwa makubaliano kati ya Iran na Marekani; (ninaamini kwamba) Tehran pia iko tayari kusaini makubaliano hayo."
(last modified 2025-11-19T02:49:32+00:00 )
Nov 19, 2025 02:49 UTC
  • Bin Salman: Tunajaribu kupatanisha baina ya Iran na Marekani

Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia ambaye kimsingi ndiye kiongozi nambari moja wa nchi hiyo amesema: "Tutafanya kila tunavyoweza kuhakikisha kunafikiwa makubaliano kati ya Iran na Marekani; (ninaamini kwamba) Tehran pia iko tayari kusaini makubaliano hayo."

Mohammad bin Salman amesema hayo wakati wa mazungumzo yake na rais wa Marekani, Donald Trump mjini New York na kuongeza kuwa, Saudi Arabia imeandaa mpango mpya wa uwekezaji wa dola trilioni 1 nchini Marekani. Amesema: "Tutaongeza uwekezaji wa Saudia nchini Marekani hadi takriban dola trilioni 1."

Katika mazungumzo hayo, Bin Salman amedai kuwa Trump amefanya kazi nzuri ya kuleta kile alichodai ni amani duniani na kuelezea matumaini yake kwamba Saudi Arabia na Marekani zinaweza "kujenga mustakabali wa pamoja chini ya kivuli cha 'amani' duniani."

Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia pia amesema kuwa nchi yake itaanza kushirikiana na Marekani katika teknolojia mpya ya Akili Unde (Artificial Intelligence - AI).

Kuhusu uhusiano wa kikanda, Bin Salman amesema kwamba Riyadh iko tayari kuwa sehemu ya Makubaliano ya Abraham (maelewano na utawala wa Kizayuni), lakini akasisitiza kwamba suala hilo linategemea "kupatikana suluhisho la mataifa mawili na kuanzishwa nchi huru ya Palestina."

Katika sehemu nyingine ya maelezo yake, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia amezungumzia jitihada zake za upatanishi kati ya Tehran na Washington, na kuongeza kwa kusema: "Tutafanya kila tuwezavyo kuhakikisha kunafikiwa makubaliano kati ya Iran na Marekani, kwa sababu Tehran pia iko tayari kusaini makubaliano hayo."

Ni vyema kukumbusha hapa kwamba, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba tofauti baina ya Iran na Marekani ni tofauti za kimsingi na kimuundo, si tofauti za kimitazamo tu.