Onyo la Afrika Kusini kuhusu njama ya kuwahamisha Wapalestina kwa nguvu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Ronald Lamola, amesema kuwasili Johannesburg wiki iliyopita kwa ndege iliyobeba wakimbizi wa Kipalestina ni “operesheni iliyopangwa waziwazi” ya kuwahamisha Wapalestina.
Lamola aliwaambia waandishi wa habari kwamba safari hiyo ya ndege inaonekana kuwa sehemu ya “ajenda pana” ya kuwahamisha Wapalestina kutoka Palestina hadi nchi mbalimbali. Alisema: “Ni operesheni iliyopangwa kwa sababu hawatumwi Afrika Kusini pekee. Kuna nchi nyingine ambako ndege kama hizo zimepelekwa.”
Waziri huyo aliongeza kuwa serikali ina mashaka kuhusu mazingira ya kuwasili kwa ndege hiyo na kwamba suala hilo linachunguzwa. Alisema: “Hatutaki ndege zaidi kuja kwetu kwa sababu hii ni ajenda ya wazi ya kuwatokomeza Wapalestina kutoka Gaza na Ukingo wa Magharibi.”
Lamola alibainisha kuwa taarifa zilizopo zinaonyesha abiria hawakuwa na vibali vinavyohitajika, lakini uchunguzi unaendelea na mamlaka zitabaini ukweli kamili, huku matokeo ya kina yakitarajiwa.
Alhamisi iliyopita, Afrika Kusini ilitoa msamaha wa viza ya siku 90 kwa Wapalestina 153 waliowasili kutafuta hifadhi nchini humo, ingawa awali walikataliwa kuingia kutokana na kukosa nyaraka za kusafiri na mihuri ya kuondoka iliyozoeleka kwenye pasi zao. Ndege yao ilitua kwa muda nchini Kenya kabla ya kuelekea Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa gazeti la kila siku la Israel, Haaretz, chama kinachoendeshwa na mtu mwenye uraia wa Israel na Estonia kinauza nafasi kwa Wapalestina wa Gaza kwenye ndege za kukodiwa kuelekea nchi za mbali kama Indonesia, Malaysia na Afrika Kusini kwa takribani dola 2,000. Israel awali ilikuwa imejadili na nchi kadhaa, ikiwemo Sudan Kusini, uwezekano wa kuwahamisha Wapalestina huko.
Mkutano na waandishi wa habari ulifanyika wakati Afrika Kusini, ambayo kwa sasa inashikilia urais wa G20 — ikiwa taifa la kwanza la Kiafrika kuwa mwanachama wa kundi la nchi tajiri zaidi duniani — inajitayarisha kuandaa Mkutano wa Viongozi wa G20 tarehe 22–23 Novemba mjini Johannesburg.
Rais wa Marekani Donald Trump awali alisema hakuna maafisa wa Marekani watakaohudhuria mkutano huo, akishutumu taifa hilo lenye viwanda vingi zaidi barani Afrika kwa “uvunjaji wa haki za binadamu” dhidi ya jamii ya wazungu makaburu wanaojulikana kama Afrikaner.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa hatua ya Marekani kutohudhuria mkutano wa G20 mjini Johannesburg ni hasara kwa Wamarekani.