Iran yapendekeza mfumo wa malipo wa kidijitali katika Jumuiya ya Shanghai
Mohammad Reza Aref Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amependekeza kuanzisha mfumo wa pamoja wa malipo ya kidijitali ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi 10 wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO).
Mfumo huo wa malipo wa kidijitali au Cryptocurrency ni mfumo ambao unamuwezesha mtu yoyote mahali popote kutuma na kupokea malipo kupitia mfumo wa mtandaoni.
Akizungumza katika Mkutano wa 24 wa Wakuu wa Serikali (Mawaziri Wakuu) wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai jana Jumanne huko Moscow, mji mkuu wa Russia, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran alitilia mkazo kwamba kutekelezwa mfumo huo wa malipo ya kidijitali kunaweza kurahisisha ubadilishanaji wa kiuchumi, kuongeza uaminifu, na kuongeza uwazi kati ya nchi wanachama wa SCO, na hivyo kukuza ushirikiano wa kikanda na kusaidia malengo ya maendeleo endelevu.
Mohammad Reza Aref pia ametoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Shanghai kushirikiana ili kuanzisha mifumo bora zaidi ya utumaji ujumbe baina ya benki mbalimbali.
Aref ameashiria haja ya kuwepo mfumo huru wa kifedha na kueleza kuwa mabadiliko ya haraka katika uchumi wa dunia yanahitajia uwepo wa mifumo ya kifedha ya kikanda ili kukabiliana na mashinikizo ya nchi za Magharibi ambayo kwa mifumo ya benki ya kimataifa.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amesisitiza kuwa Iran inaunga mkono kikamilifu kuanzishwa Benki ya Maendeleo ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) ili kufadhili miradi ya miundomsingi na kupunguza utegemezi kwa mifumo ya fedha ya kimataifa isiyo ya kiadilifu.