Trump asema huenda akaishambulia kijeshi Mexico
Rais wa Marekani Donald Trump ametaja uwezekano wa kuanzisha mashambulizi ya kijeshi nchini Mexico kwa madai ya eti kukabiliana na magenge ya dawa za kulevya.
Trump ametoa kauli hiyo ya kichokozi akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House Jumatatu, Trump alipokuwa akijibu swali kuhusu uwezekano wa kulenga Mexico kijeshi.
Kuhusu iwapo mashambulizi yangefanywa kwa ridhaa ya Mexico pekee, Trump alisema hatalijibu swali hilo. Aliongeza kuwa amekuwa akizungumza na serikali ya Mexico na kwamba taifa hilo linafahamu msimamo wake.
Katikati ya maelezo yake Jumatatu kuhusu Mexico, Trump aligeukia Colombia, na kusema kuwa anatafakari pia kulenga kijeshi vituo alivyovotaja kuwa vya mihadarati nchini humo.
Trumpa katika wiki za hivi karibuni ametoa matamko ya kichokozi ya kutaka kuishambulia Venezuela kijeshi kwa ajili ya eti kukabiliana na magenge ya dawa za kulevya.
Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, amesisitiza kuwa ulimwengu mzima unafahamu kuwa mabepari wanaotawala Marekani wanataka kupora mafuta, gesi na dhahabu ya nchi yake.
Amesema Marekani inadai kuwa inataka kuivamia Venezuela kwa ajili ya kukabiliana na mihadarati lakini jambo ambalo liko wazi ni kuwa hakuna ukweli katika madai yao na wanafahamu vyema nukta hiyo.
Hivi karibuni Marekani ilituma meli ya kivita ya kubeba ndege, USS Gerald R. Ford , ambayo ndiyo kubwa zaidi duniani, pamoja na meli zingine tano za kivita kwenda Amerika ya Kusini, hatua ambayo imekosolewa vikali na Venezuela ikiitaja kuwa ya kichokozi, hatarishi, na kinyume cha sheria za kimataifa.