Afrika Kusini yaanza kufufua miradi ya nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133284-afrika_kusini_yaanza_kufufua_miradi_ya_nyuklia
Afrika Kusini imeamua kufufua miradi ya nyuklia iliyokwama kwa muda mrefu na kufungua tena vituo muhimu vya utafiti, kama sehemu ya juhudi za kujenga upya utaalamu wa ndani na kujipanga upya katika masoko yanayochipuka ya mafuta ya mitambo ya nyuklia duniani.
(last modified 2025-11-17T09:16:11+00:00 )
Nov 17, 2025 09:14 UTC
  • Afrika Kusini yaanza kufufua miradi ya nyuklia

Afrika Kusini imeamua kufufua miradi ya nyuklia iliyokwama kwa muda mrefu na kufungua tena vituo muhimu vya utafiti, kama sehemu ya juhudi za kujenga upya utaalamu wa ndani na kujipanga upya katika masoko yanayochipuka ya mafuta ya mitambo ya nyuklia duniani.

Hayo yamedokezwa Jumapili na Waziri wa Nishati Kgosientsho Ramokgopa.

Akikiri changamoto zilizopita na kupotea kwa wahandisi wenye ujuzi, waziri amesema Afrika Kusini inafungua tena maabara za maendeleo ya mafuta na kujenga kizazi kipya cha wanasayansi wa nyuklia kwa kushirikiana na vyuo vikuu.

Ramokgopa amesema, chini ya uongozi wa Shirika la Nishati ya Nyuklia la Afrika Kusini (NECSA), nchi hiyo “itajenga upya mpango wa nyuklia na ajenda ya utafiti”

Aidha, alibainisha kuwa serikali itaanzisha tena vituo muhimu, ikiwemo maabara ya kupima mafuta ya nyuklia na maeneo ya majaribio ya gesi ya helium, hatua inayolenga kuifanya Afrika Kusini kuwa mhusika mkubwa katika utafiti na maendeleo ya mafuta ya nyuklia.

Akiashiria China, Ramokgopa alisema kwa sasa kuna nchi moja pekee inayosambaza mafuta kwa mitambo ya joto la juu. Ameongeza kuwa China, ikiwa muuzaji mkubwa duniani, itakidhi mahitaji yake ya ndani kadri mitambo mipya itakavyoanza kufanya kazi na tayari ipo katika nafasi ya kuongoza soko linalokua la Small Modular Reactor (SMR).

Amesisitiza kuwa Afrika Kusini inarejea katika nafasi yake halisi kama mhusika mkubwa katika sekta ya mafuta ya nyuklia, na kwa muda, “tutakuwa mhusika asiyeweza kuepukika katika nyanja ya nyuklia.”

Ramokgopa ameongeza kuwa serikali imetoa mtaji wa randi bilioni 1.2 za Afrika Kusini (takribani dola milioni 70) kwa Shirika la Nishati ya Nyuklia la Afrika Kusini, na inapanga kushirikisha wadau wengine ili kupanua uwezo wa nyuklia, ikijenga uzalishaji wa ndani wa takribani Giga Wati 5.2.

Afrika Kusini ndiyo nchi pekee barani Afrika yenye kituo cha umeme wa nyuklia kinachojulikana kama Koeberg.