Pep Guardiola awataka Wahispania kushikamana na Palestina
-
Pep Guardiola awataka Wahispania kushikamana na Palestina
Kocha wa Manchester City Mhispania Pep Guardiola, amewataka wananchi wa Uhispania kuonyesha mshikamano na wananchi wa Palestina.
Katika ujumbe wake wa video, amewataka watu wa Uhispania na mashabiki wa Barcelona kuonyesha mshikamano wao na watu wa Palestina na mashahidi wa vita vya Gaza kwa kuhudhuria mechi ya hisani kati ya timu ya Catalonia na timu ya taifa ya Palestina.
Meneja wa Manchester City Pep Guardiola ametoa ujumbe kabla ya mechi ya kirafiki ya hisani kati ya timu ya Catalonia na timu ya taifa ya Palestina Jumanne ijayo ya tarehe 18 Novemba kwenye Uwanja wa Olimpiki huko Barcelona, akiwahimiza mashabiki kuhudhuria mechi hiyo kwa wingi.
"Barcelona, mji wa amani, utaandaa mechi kati ya timu ya taifa ya Catalonia na timu ya taifa ya Palestina. Mechi hii inaenda zaidi ya soka na ni sauti ya mshikamano na heshima kwa wanamichezo zaidi ya 400 wa Palestina waliofariki Gaza. Hebu tujaze uwanja," alisema katika ujumbe huo wa video.
Kocha huyo Mhispania amewahi mara kadhaa kuwaunga mkono watu wa Gaza na Palestina na kuonyesha misimamo dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni.
Hivi karibuni kocha huyo wa timu ya soka ya Manchester City alikosoa vikali ukimya wa walimwengu kuhusiana na jinai za utawala wa kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kusema: "Ubinadamu umetoweka."
Akiashiria Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia, Pep Guardiola alisema, "Hapo zamani, majanga yaliendelea kufichwa, lakini leo tunaona kila kitu mubashara kwenye televisheni, lakini hatuna majibu hata kidogo."