Walimwengu walaani Wazayuni kuchoma moto msikiti katika Ukingo wa Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i133240-walimwengu_walaani_wazayuni_kuchoma_moto_msikiti_katika_ukingo_wa_magharibi
Hatua ya kundi la walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya kufurutu ada ya kuchoma msikiti wa Hajja Hamida katika Ukingo wa Magharibi huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu imelaaniwa katika kila kona ya dunia.
(last modified 2025-11-16T07:06:32+00:00 )
Nov 16, 2025 07:06 UTC
  • Walimwengu walaani Wazayuni kuchoma moto msikiti katika Ukingo wa Magharibi
    Walimwengu walaani Wazayuni kuchoma moto msikiti katika Ukingo wa Magharibi

Hatua ya kundi la walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya kufurutu ada ya kuchoma msikiti wa Hajja Hamida katika Ukingo wa Magharibi huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu imelaaniwa katika kila kona ya dunia.

Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar nchini Misri kimetangaza katika taarifa yake kwamba hatua hii inaakisi tabia ya kishenzi ya watu wenye misimamo mikali ambao hawaheshimu matukufu ya nyumba za Mwenyezi Mungu na wanadhihirisha misimamo yao mikali ya chuki dhidi ya kila kitu cha Kiislamu.

Walowezi hao wa Kizayuni waliteketeza kwa moto Msikiti wa Hajja Hamida ulioko kijiji cha Deir Istiya, kaskazini-magharibi mwa mji wa Salfit, alfajiri ya Akhamisi.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alisema taasisi hiyo ya kimataifa “inakemea vikali” shambulio hilo.

“Maeneo ya ibada lazima yaheshimiwe na kulindwa kila wakati,” alisema Stephane Dujarric akiwaeleza waandishi wa habari katika makao makuu ya UN mjini New York.

Jordan kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Wakimbizi pia ilikemea vikali mashambulio ya walowezi wa Kiyahudi. Msemaji wa wizara hiyo, Fouad Majali, alisisitiza msimamo wa Amman wa kukataa mashambulio hayo, akiyataja kama “mwendelezo wa sera za misimamo mikali za utawala wa Israel na kauli za maafisa wake zinazochochea chuki na ukatili dhidi ya watu wa Palestina.”

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uswisi pia ilieleza wasiwasi mkubwa juu ya ongezeko la ukatili wa walowezi wa Kiyahudi dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi.