Charlotte Slente: Zaidi ya nusu ya Wasudan wanahitaji msaada wa kibinadamu
-
Zaidi ya nusu ya Wasudan wanahitaji msaada wa kibinadamu
Zaidi ya nusu ya idadi ya watu wa Sudan wanahitaji msaada wa kibinadamu. Hayo yameelezwa na Mkuu wa Baraza la Wakimbizi la Denmark, huku mapigano yakiliharibu taifa hilo la kaskazini mashariki mwa Afrika.
Katibu Mkuu wa Baraza la Wakimbizi la Denmark Charlotte Slente ameziambia duru za habari baada ya ziara yake katika eneo la mpakani mwa Chad na Sudan na kusema alishuhudia hali ambayo zaidi ya watu milioni 30 wanahitaji msaada wa kibinadamu, hiyo ikiwa ni nusu ya idadi jumla ya watu wa Sudan na kusisitiza kuwa "mateso aliyoyashuhudia hayafikiriki."
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema ana wasiwasi mkubwa kutokana na ripoti za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na mauaji ya halaiki mjini El Fasher, pamoja na kuongezeka mapigano katika maeneo ya Kordofan.
Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM) limetaka kuchukuliwa hatua za haraka ili kuwasaidia mamilioni ya raia walioathiriwa na vita vya Sudan kati ya jeshi la nchi hiyo na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
Jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF wanapigana vita tangu Aprili 15, 2023, vita ambavyo vimeshindwa kuhitimishwa kupitia upatanishi wa kikanda na kimataifa. Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine wamekuwa wakimbizi kutokana na mgogoro wa Sudan.
Mashirika ya ndani ya Sudan na ya kimataifa yanasema kuwa hali ya mambo ilizidi kuwa mbaya mwishoni mwa mwezi uliopita wakati kikosi cha RSF kilipouteka mji wa El-Fasher ambao ni makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini na kufanya mauaji ya halaiki ya kikabila.