Hamas yatahadharisha kushadidi janga la kibinadamu Ukanda wa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i133238-hamas_yatahadharisha_kushadidi_janga_la_kibinadamu_ukanda_wa_gaza
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeonya kuhusiana na kushadidi janga la kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-11-16T09:06:38+00:00 )
Nov 16, 2025 07:05 UTC
  • Hamas yatahadharisha kushadidi janga la kibinadamu Ukanda wa Gaza
    Hamas yatahadharisha kushadidi janga la kibinadamu Ukanda wa Gaza

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeonya kuhusiana na kushadidi janga la kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Onyo hilo limetolewa na msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ambaye ametahadharisha kuhusu kushadidi maafa ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza kufuatia mvua zilizonyesha hivi karibuni.

Siku ya Jumamosi, msemaji wa Hamas Hazem Qassem alitoa wito wa kuwepo kwa msimamo wa mara moja na madhubuti wa taasisi za kimataifa za Kiislamu na Kiarabu, akieleza kuzidi kwa hali isiyovumilika katika Ukanda wa Gaza baada ya mvua za hivi karibuni.

Msemaji wa Hamas anaonya kwamba maafa ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza yamechukua mwelekeo mbaya zaidi sambamba na kuwadia majira ya baridi; hali hii inahitaji uchukuaji hatua za wazi na za haraka kutoka kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu kwa kuzingatia nyaraka za uanzilishwaji wa taasisi hizi.

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) nalo limetangaza kuwa, mvua kubwa iliyonyesha katika Ukanda wa Gaza imefanya hali ya kibinadamu kuwa ngumu zaidi, huku familia nyingi zikipata hifadhi katika eneo lolote linalowezekana, ikiwa ni pamoja na mahema ya muda.

UNRWA imesisitiza kuwa, kuna hitajio la dharura na muhimu la vifaa vya makazi na vifaa vingine huko Gaza, na kwamba vifaa hivi viko mikononi mwa shirika hilo, lakini inahitajika idhini ya ufikiaji ili kuvipeleka kwa watu wenye kuhitajia.