Katibu Mkuu wa UN: Ugaidi katika eneo la Sahel ni tishio linaloongezeka
-
Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewatahadharisha viongozi duniani kwamba ugaidi katika eneo la Sahel barani Afrika ni tishio linaloongezeka duniani.
Antonio Guterres amezitaka nchi za eneo la Sahel kushirikiana na kuchukua hatua za pamoja dhidi ya ugaidi. Guterres ameeleza haya katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
"Tunakabiliwa na hatari ya athari mbaya katika eneo lote la Sahel. Nchi nyingi zinayumbayumba," amesema Guterres na kuongeza kuwa dunia inahitaji kushikamana na watu wa eneo la Sahel. Vilevile ametoa mwito kwa wanachama wa Baraza la Usalama kulisaidia eneo hilo la Afrika.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameashiria pia mgogoro wa usalama huko Mali ambapo kundi la wanagambo wa JNIM wamekuwa wakivuruga usambazaji wa mafuta.
Uamuzi wa karibuni wa Burkina Faso, Mali na Niger wa kujitoa katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) umesababisha changamoto mpya ka ushirikiano wa kanda hiyo.
Kuhusu suala hilo, Mkuu wa Tume ya ECOWAS, Omar Alieu Touray amesema: "Kwa bahati mbaya, hali ya mambo katika eneo la Sahel haiaminiki."
Touray amezitolea wito nchi wanachama wa Baraza la Usalama la UN kulisaidia eneo la Sahel kujenga hali ya kuaminiana. Amesema, si pesa wala suhula ambazo zitazisaidia nchi za Sahel kutokomeza ugaidi iwapo hazitashirikiana.
Eneo la Sahel linachangia zaidi ya nusu ya vifo vyote vinavyosababishwa na hujuma za kigaidi duniani, na hivyo kulifanya kuwa kitovu cha kimataifa cha ugaidi. Ripoti hii ni kwa mujibu wa data za kimataifa kuhusu ugaidi.