Iran: Azimio la Marekani lililopasishwa na UN kuhusu Gaza linahalalisha ukaliaji mabavu
-
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran
Iran imekosoa azimio lililoandaliwa na Marekani na kupasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaloweka utaratibu wa kutumwa Gaza usimamizi wa nchi ajinabi na kutahadharisha kuwa azimio hilo linadhoofisha haki za msingi za watu wa Palestina.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema katika taarifa yake kuwa waratibu wa azimio hilo "wamepuuza kwa makusudi jukumu kuu la Umoja wa Mataifa na maazimio ya awali ya umoja huo kuhusu Palestina.
Azimio nambari 2803 lililopasishwa Jumatatu wiki hii limeunga mkono kuanzishwa kwa "Kikosi cha Kimataifa cha Kulinda Amani (ISF)" huko Gaza kwa mujibu wa mpango wa vipengee 20 wa Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye amedai kuwa mpango huo unalenga kukomesha vita vya mauaji ya kimbari ya utawala wa Israel dhidi ya Gaza vilivyoanza Oktoba 2023.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeeleza "wasiwasi mkubwa" kuhusu azimio hilo, ikisisitiza kuwa Iran inaunga mkono mpango wowote wa kikanda au kimataifa unaolenga kukomesha mauaji ya kimbari ya Israel na jinai zinazofanyika katika Ukanda Gaza, kurahisisha misaada ya kibinadamu na kuhakikisha kuwa wanajeshi vamizi wa Israel wanaondoka kikamilifu katika ukanda huo.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeongeza kuwa: Sehemu za azimio hilo imeainisha uwepo wa mfumo wa usimamizi kwa ajili ya Gaza, hatua inayowapora "Wapalestina haki zao za msingi, hasa haki ya kujitawala na kuunda nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa Baitul Muqaddas.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia imetahadharisha kuwa kupasishwa kwa azimio lililopendekezwa na Marekani kunahalalisha kuendelea kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu Ukanda wa Gaza, kugawanywa ukanda huo au kuutenganisha na jiografia ya Palestina, hatua ambayo inaweza kuwa na "matokeo hatari."
Azimio hilo limepingwa pia na harakati na makundi ya kupigania ukombozi ya Palestina. Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imepinga vikali azimio hilo, ikisema kwamba linalazimisha usimamizi wa kimataifa katika eneo hilo la Palestina. Taarifa iliyotolewa na Hamas imesema azimio hilo la UN halikidhi matakwa na haki za kisiasa na kibinadamu za watu wa Palestina.
Harakati hiyo imesisitiza kwamba kikosi chochote cha kimataifa kinapaswa kipelekwe kwenye mipaka ya Gaza pekee ili kufuatilia usitishaji mapigano chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.
"Kukipa kikosi cha kimataifa majukumu ndani ya Ukanda wa Gaza, ikiwa ni pamoja na kupokonya silaha za makundi ya mapambano, kunakipokonya sifa ya kutopendelea upande wowote, na kukifanya sehemu ya mzozo kwa niaba ya utawala vamizi," imesema taarifa ya Hamas.
Russia, China na baadhi ya mataifa ya Kiarabu yalipinga pendekezo hilo, yakitaja wasiwasi kuhusu bodi ambayo bado haijaanzishwa itakayosimamia eneo hilo kwa muda na kutokuwepo jukumu lolote la mpito kwa Mamlaka ya Palestina.