Grossi: Wakaguzi wa wakala wa IAEA wamerejea Iran
-
Rafael Grossi
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amesema katika kikao cha robo mwaka cha Bodi ya Magavana ya wakala huo kwamba: "Wakaguzi wa IAEA wamerejea Iran na wamefanya ukaguzi katika vituo ambavyo havikuathiriwa na mashambulizi ya Juni, lakini ushirikishwaji zaidi unahitajika ili kurejesha ukaguzi kamili."
Kwa mujibu wa IRNA, Rafael Grossi amesema leo katika kikao cha Bodi ya Magavana ya IAEA kwamba: "Wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki wamerejea katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wamefanya ukaguzi na uhakiki wa taarifa za muundo katika aghalabu ya vituo mbavyo havikuharibiwa na mashambulizi ya kijeshi ya Juni."
Grossi amesema ushirikishwaji zaidi unahitajika ili kurejesha ukaguzi kamili, ikiwa ni pamoja na katika maeneo yaliyoathiriwa, ili Iran iweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia, NPT.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki amesema anawasiliana mara kwa mara na Tehran na kwamba anaiomba Iran iuwezeshe wakala huo kuzifikia taasisi zake zilizoathiriwa na mashambulizi hususan kuifikia akiba yake ya madini ya urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha chini (LEU), na ile iliyorutubishwa kwa kiwango cha juu (HEU)."
Inafaa kuashiria kuwa ushirikiano kati ya Tehran na IAEA ulikumbwa na vizuizi kufuatia mashambulizi haramu ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran vinavyoendesha shughuli zake kwa malengo ya amani.