Umri wa unywaji pombe Kenya wapendekezwa kuongezwa kutoka miaka 18 hadi 21
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128436-umri_wa_unywaji_pombe_kenya_wapendekezwa_kuongezwa_kutoka_miaka_18_hadi_21
Mamlaka ya Taifa ya Kupambana na Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya nchini Kenya (NACADA) imetetea pendekezo lake la kutaka umri wa kisheria wa kunywa pombe nchini humo uongezwe kutoka miaka 18 hadi 21, ikitaja utafiti wa kiafya, maoni ya umma na viwango vya kimataifa kama msingi wa pendekezo hilo.
(last modified 2025-07-17T12:04:25+00:00 )
Jul 17, 2025 11:37 UTC
  • Umri wa unywaji pombe Kenya wapendekezwa kuongezwa kutoka miaka 18 hadi 21

Mamlaka ya Taifa ya Kupambana na Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya nchini Kenya (NACADA) imetetea pendekezo lake la kutaka umri wa kisheria wa kunywa pombe nchini humo uongezwe kutoka miaka 18 hadi 21, ikitaja utafiti wa kiafya, maoni ya umma na viwango vya kimataifa kama msingi wa pendekezo hilo.

Naibu Mkurugenzi wa Mipango wa NACADA, Bw Kirwa Lelei, amesema hatua hiyo inalingana na mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ambayo yanalenga kulinda afya na maendeleo ya vijana.

Amefafanua kuwa NACADA iliandaa mikutano ya kushirikisha umma katika maeneo 10 ya nchi, ambapo maeneo manane yaliunga mkono kupandishwa kwa umri wa chini wa kunywa pombe hadi miaka 21. Maeneo ya Mombasa na Kaskazini yalisema umri huo upandishwe hadi miaka 25.

Wataalamu wa afya na wanasaikolojia wanaunga mkono pendekezo hilo wakisema ubongo wa binadamu huwa unaendelea kukua hadi kufikia takriban miaka 25. Kuanza pombe mapema kunawaweka vijana katika hatari ya kutekwa na uraibu, hasa kwa walio chini ya miaka 18 ambao wanalewa kutokana na ushawishi wa marafiki na upatikanaji rahisi wa pombe.

Takwimu mpya zilizotokana na utafiti uliofanywa na NACADA zinaonyesha hali ya kutia wasiwasi baada ya kubainika kuwa asilimia 2.6 ya wanafunzi wa shule za msingi wamewahi kunywa pombe, asilimia 3.8 kati ya wanafunzi wa sekondari, asilimia 18 wa vyuo vikuu, huku asilimia 23.8 ikirekodiwa miongoni mwa watumishi wa umma. Lelei amesema wanafunzi wa vyuo vikuu ndio wanaoathirika zaidi na unywaji wa pombe.

“Hizi takwimu ni za kushtua na zinaonyesha kwa nini ni muhimu kuzuia mapema,” ameeleza Lelei.

Kwa mujibu wa afisa huyo wa NACADA, katika kuimarisha utekelezaji hasa katika vyuo vikuu ambako kuna matumizi ya juu ya pombe, taasisi hiyo inapanga kushirikiana na wakuu wa vyuo, wachungaji na viongozi wa kidini ili kupambana na ongezeko la uraibu miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Kenya.../